Shule ya mfano masomo ya Sayansi kuanzishwa Arusha

Muktasari:

Jiwe la msingi la Shule ya Sekondari Mrisho Gambo ya mkoani Arusha limewekwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania, Profesa Joyce Ndalichako na Balozi wa China nchini humo, WANG  Ke ambapo itakuwa inatoa masomo ya sayansi kwa sehemu kubwa.

Arusha. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania, Profesa Joyce Ndalichako na Balozi wa China nchini humo, WANG  Ke wameshiriki uwekezaji wa jiwe la msingi la Shule ya Sekondari Mrisho Gambo ya mfano ya masomo ya Sayansi mkoani Arusha.

Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amepokea viongozi hao leo Alhamisi Januari 16,2020 katika hafla iliyofanyika shuleni hapo ikiwa ni mikakati ya Mkoa wa Arusha, kuboresha sekta ya elimu nchini.

Amesema shule hiyo, iliyopewa jina la Mrisho Gambo sekondari ipo katika Kata ya Olasiti katika Jiji la Arusha, ambapo hadi sasa tayari madarasa manane ya kisasa yamekamilika, maabara nne, chumba cha  Kompyuta, nyumba za walimu na madawati.

"Tunataka shule hii iwe ya mfano, itakuwa ikichukua wanafunzi wa sayansi kwa kiasi kikubwa ili kusaidia  kupata wataalam wakutosha katika sayansi na teknolojia," amesema Gambo

Wakizungumza baada ya kutembelea shule hiyo, Waziri Ndalichako na Balozi Wang Ke, wamepongeza jitihada za kukuza elimu ambazo zinafanywa na Gambo na wasaidizi wake.

Waziri Ndalichako amesema anapongeza jitihada za kukuza elimu mkoa wa Arusha ambao umekuwa ukifanya vizuri katika mitihani.

Naye Wang Ke amesema Serikali ya China inaendelea kushirikiana na mkoa wa Arusha katika kuboresha elimu, ambapo katika shule hiyo kampuni tatu za China zimechangia ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu, kompyuta na maabara mbili.

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Catherine Magige ameahidi kutoa gari aina ya Noah kwa shule hiyo.

Shule hiyo, imejengwa kwa mchango wa taasisi mbalimbali, ikiwapo Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro, Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Ubalozi wa china, Benki ya CRDB, I& M Bank, Benki ya NMB, Kampuni ya Tanalec, kampuni za utalii na Jiji la Arusha.