Shule yasema haina taarifa tukio la mwanafunzi aliyejiua kwa kujipiga risasi

Muktasari:

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Arusha Meru, Mustapha Nassoro amesema hadi leo asubuhi Jumatatu Agosti 19, 2019 walikuwa hawajapewa taarifa za aliyekuwa mwanafunzi wa shule hiyo, Faisal Salimu (19) kujiua kwa kujipiga risasi.


Arusha. Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Arusha Meru, Mustapha Nassoro amesema hadi leo asubuhi Jumatatu Agosti 19, 2019 walikuwa hawajapewa taarifa za aliyekuwa mwanafunzi wa shule hiyo, Faisal Salimu (19) kujiua kwa kujipiga risasi.

Mwanafunzi huyo amejipiga risasi kwa kutumia bunduki ya baba yake Salimu Ibrahim (59) aina ya Rifle Winchester akiwa amejifungia chumbani kwake katika nyumba ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) eneo la Soko Kuu jijini Arusha nchini Tanzania.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu amesema taarifa za kifo cha mwanafunzi huyo aliyejiua jana Jumapili wamezisikia kupitia vyombo vya habari.

“Taarifa hii imetushtusha kwa kuwa tumeisikia kupitia vyombo vya habari lakini tunajiandaa kwenda nyumbani. Alikuwa akisoma kidato cha tano. Shule tutatoa taarifa rasmi Jumatano kuhusu tukio hili,” amesema.

Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Jonathan Shani amesema katika tukio hilo lilitokea Jumapili saa 11 alfajiri, mwanafunzi huyo alijipiga risasi katika paji la uso.

Uchunguzi wa awali umebaini mwanafunzi huyo alikuwa anasumbuliwa na msongo wa mawazo kutokana na kushutumiwa kuwa anatumia dawa za kulevya.

"Tumeanza uchunguzi wa tukio hili na silaha hii kama ilikuwa inamilikiwa kihalali. Hatua za kisheria zitachukuliwa ikibainika kama silaha haikuhifadhiwa vizuri," amesema Shana.

Jirani wa nyumba huyo, Ahmed Issa amesema mwanafunzi huyo alifariki akiwa njiani wakati anapelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mountmeru.

"Tukio hili lilifanywa siri sana, hata sisi majirani tumepata taarifa usiku huu," amesma jirani huyo.