VIDEO: Shule yazungumzia deni la Sh550,000 la aliyeongoza matokeo darasa la saba

Muktasari:

Uongozi wa  Shule ya Graiyaki aliyokuwa akisoma mwanafunzi aliyeshika nafasi ya kwanza katika mtihani wa kumaliza darasa la saba, Grace Manga umesema haukuona tatizo kumruhusu afanye mtihani licha ya kuwa na deni kubwa la ada.


Serengeti. Uongozi wa  Shule ya Graiyaki aliyokuwa akisoma mwanafunzi aliyeshika nafasi ya kwanza katika mtihani wa kumaliza darasa la saba, Grace Manga umesema haukuona tatizo kumruhusu afanye mtihani licha ya kuwa na deni kubwa la ada.

Meneja wa shule hiyo, Grace Godfrey amesema anamfahamu mama wa mwanafunzi huyo na hana historia ya kutolipa ada. Alikuwa akidaiwa zaidi ya Sh550,000.

 “Si Grace tu wapo watoto wengi wanamaliza wana madeni, lakini kwa kuwa tumekuwa nao miaka saba nawafahamu.”

“Wazazi wanapoomba kuwa watoto wasome watalipa hakuna haja ya kumkatili  mtoto, sasa ningetanguliza mahitaji ya fedha leo Grace angekuwa wapi? Haya ni mambo ya msingi sana unapokuwa unatoa huduma,” amesema Grace.

Amesema Shule zake zinapokea watoto wanaotoka familia zenye uwezo tofauti na  kwa uzoefu wake anajitahidi kuwaelewa wazazi na kujua tabia zao.

"Sisi tunaangalia pia nia ya mtu kuleta mtoto na hali yake, tunawasikiliza wazazi na kuwavumilia ,”amesema.

Kuhusu kulipwa kwa deni hilo la Sh550,000 , amesema  lilishalipwa baada ya  Grace kumaliza mitihani.