Shule zilizoingia 10 bora darasa la saba 2019 hizi hapa

Muktasari:

  • Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) nchini Tanzania jana Jumanne Oktoba 15, 2019 ilitangaza matokeo ya mtihani wa darasa la saba uliofanyika Septemba 11 na 12, 2019.

Dar es Salaam. Shule sita za msingi nchini Tanzania zimeingia kwenye orodha ya shule 10 bora kitaifa kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mitano iliyopita zikishindana na shule ambazo zimekuwa zikitawala kwenye orodha hiyo.

Shule hizo ambazo zote zinapatikana Kanda ya Ziwa ni Graiyaki (Mara), Musabe (Mwanza), Tulele (Mwanza), Kemebos (Kagera), Little Treasures (Shinyanga) na Peaceland (Mwanza).

Shule ya Graiyaki imeshika nafasi ya kwanza kitaifa huku ikiwa imetoa wanafunzi sita ambao wameingia kwenye orodha ya wanafunzi 10 bora kitaifa, wavulana wakiwa watatu ambao ni Victor Godfrey, Aziz Yassin na Goldie Hhayuma; na wasichana ni Grace Manga, Nyanswi Richard na Neema Mushi. Pia, Grace ameongoza kitaifa.

Shule nyingine nne za Twibhoki, Mugini, Kwema Modern na Rocken Hill ambazo zimeingia kwenye orodha ya shule 10 bora mwaka 2019, zimewahi kuingia kwenye orodha hiyo zaidi ya mara moja katika miaka mitano iliyopita.

Shule ya msingi Rocken Hill imefanikiwa kuingia kwenye orodha ya shule 10 bora kitaifa mara nne katika kipindi cha miaka mitano iliyopita huku ikishindwa kuingia katika orodha hiyo mwaka 2017 pekee.

Shule zinazoifuatia Rocken Hill ni pamoja na shule ya Twibhoki (Mara) ambayo iliingia mwaka 2015, 2018 na 2019; Mugini ya Mwanza (mwaka 2015, 2016 na 2019) na Kwema Modern ya Shinyanga (mwaka 2016, 2018 na 2019).

Katika matokeo ya mwaka 2019 yaliyotangazwa jana Jumanne Oktoba 15,2019 shule 10 zilizoongoza kitaifa ni Graiyaki (Mara), Twibhoki (Mara), Kemebos (Kagera), Little Treasures (Shinyanga), Musabe (Mwanza), Tulele (Mwanza), Kwema Morden (Shinyanga), Peaceland (Mwanza), Mugini (Mwanza) na Rocken Hill (Shinyanga).

Kwa mwaka 2018, zilizoongoza zilikuwa ni Raskazone (Tanga), Nyamuge (Mwanza), Twibhoki (Mara), Kwema Modern na Rocken Hill (Shinyanga), St Anne Marie (Dar es Salaam), Jkibira (Kagera), St Akleus Kiwanuka (Kagera), St Severine (Kagera), Rweikiza (Kagera).

Kumi bora ya mwaka 2017 zilikuwa ni St. Peters (Kagera), St Severine (Kagera), Alliance (Mwanza), Sir. John (Tanga), Palikas (Shinyanga), Mwanga (Kagera), Hazina (Dar es salaam), St. Anne Marie (Dar es salaam), Rweikiza (Kagera) na Martin Luther (Dodoma).

Vilevile mwaka 2016, shule zilizoingia 10 bora ni Kwema Modern (Shinyanga), Rocken Hill (Shinyanga), Mugini (Mwanza), Fountain of Joy (Dar), Atlas (Dar) na Gift Skillfull (Dar), Mudio Islamic (Kilimanjaro), St. Achileus (Kagera) na Carmel (Morogoro).

Mwaka 2015 ulikuwa na shule kama vile Waja Springs (Geita), Enyamai, Twibhoki (Mara), Mugini, Rocken Hill, Karume (Kagera), Alliance (Mwanza), Little Flower (Mara), Palikas (Shinyanga) na St Caroli (Mwanza).