Siasa zilivyotawala mijadala taarifa kamati za Bunge

Wabunge wakijadiliana jambo ndani ya ukumbi wa Bunge wakati wa kikao cha saba cha mkutano wa 18 wa Bunge jijini Dodoma jana. Kuanzia kushoto Joseph Musukuma (Geita Vijijini), Venance Mwamoto (Kilolo), Abdul-Aziz Abood (Morogoro Mjini) na Goodluck Mlinga wa Ulanga. Picha na Edwin Mjwahuzi

Dodoma. Kwa mara nyingine siasa za uchama zilitawala katika mjadala wa taarifa ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, wakati wabunge wa CCM na Chadema walipokuwa wakielekeza hoja zao kwenye vyama.

Hii si mara ya kwanza kwa wabunge kujielekeza zaidi katika siasa za vyama wakati wa kujadili taarifa muhimu na hivyo kusababisha majibizano, kujaribu kukwamishana na pia kuonekana wakitaka kuyumbishana kwa kutaka miongozo na taarifa.

Jana, ambayo siku ya kumbukumbu ya kuanzishwa kwa CCM, siasa hizo zilianza katika maaswali na majibu wakati mbunge wa viti maalum, Amina Mollel alipopewa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwa Wizara ya Maliasili na Utalii Utalii.

Kabla ya kuuliza swali, mbunge huyo alianza kuimba wimbo unaoeleza CCM ilizaliwa Februari 5, 1977 na kusababisha wabunge wanaoonekana kuwa wa CCM kumpigia makofi. Alipokewa na mbunge wa Chemba, Juma Nkamia.

Hali hiyo ilifanya Spika Ndugai awatulize, akisema “tulieni kwanza, hiyo ni CCM. Vyama vingine havina hata siku ya kuzaliwa”.

Hali hiyo ilijitokeza juzi wakati wa kujadili taarifa ya Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa, Katiba na Sheria wakati wabunge wa Chadema walipoibua hoja ya kauli za vitisho vya maisha walkizodai zinatolewa na viongozi wa CCM, lakini wahusika hawachukui hatua.

Suala hilo lilifikia hatua ya mbunge wa Lema kusema kuwa “ushindi wa CCM umekuwa ukipatikana kwa kutumia mtutu wa bunduki”, hali iliyomfanya Waziri Jenister Mhagama kutaka kauli hiyo ifutwe.

Hali kama hiyo iliendelea jana wakati wa kujadili taarifa ya Kamati ya Nishati na Madini.

Ingawa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama pia iliwasilisha taarifa yake ya utekelezaji, wabunge wengi walijielekeza zaidi katika Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini huku baadhi wakitoka nje ya mjadala na kusababisha Ndugai kuwakumbusha wajikite kwenye hoja.

Spika Job Ndugai aliiambia Mwananchi baadaye kuwa haiwezekani kuzuia siasa kujitokeza katika hoja za wabunge, hasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu

“Unajua suala hilo linategemeana,” alisema Ndugai.

“Ungekuwa umenipa mfano wa wanachokisema ningeweza kukujibu, mfano ni nini?”

Alipoelezwa kuwa baadhi ya wabunge huacha kujadili hoja mathalani za kamati za Bunge zilizowasilishwa na kuanza kurushiana vijembe vya kisiasa, Ndugai alisema hayo ni masuala binafsi.

“Hayo ni mambo ya kawaida katika mabunge,” alisema.

“Maana kitu chochote mnachokifanya mwisho wa siku ni ushindani katika uchaguzi mkuu na kwa Tanzania, huwezi kuingia kwenye uchaguzi wowote bila kuwa na tiketi ya chama. Hatuna wagombea binafsi. Ni kitu cha kawaida kabisa.”

Wakati Ndugai akieleza hayo, katibu wa wabunge wa CCM, Jason Rweikiza na mnadhimu wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Ester Bulaya pia walizungumzia hali hiyo, kila mmoja akiuponda upande mwingine.

Alipoulizswa kuhusu suala hilo, Rweikiza alisema kuna namna mbili za watu wanaokwenda kinyume na hoja zilizowasilishwa na kamati.

Alisema aina ya kwanza ni wabunge ambao ni wavurugaji wanakuwa wameandaa watu wa kuwapiga picha kwa ajili ya kwenda kutuma kwenye mitandao ya kijamii.

Alisema wanafanya hayo ili waonekane kuwa wamesema sana bungeni na kwamba, hao hufikia wakati mwingine hata kuitukana Serikali.

Alitoa mfano wa michango ya jana wakati baadhi ya wabunge wa upinzani walikuwa hawaoni mafanikio yaliyofanyika katika miaka minne ya Serikali.

Alisema aina ya pili ni wabunge ambao kwa bahati mbaya hawajaelewa wanajikuta wameacha hoja husika baada ya kushindwa kujizuia.

“Hawa wanarekebishika na madhara yake si makubwa kama wale wavurugaji ambao wakati mwingine hutukana Serikali kama ilivyofanyika leo (jana),” alisema.

Lakini mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Ester Bulaya alisema hakuna mbunge anayechangia kinyume na hoja iliyowasilishwa.

Alisema kilichotokea jana na katika vikao vilivyopita, kuna hoja ambazo wabunge wengine hawataki kuzisikia na kutoa mfano wa hoja ya kampuni ya Barrick.

“Ile ilikuwa ni Kamati ya Nishati ya Madini ndiyo hoja iliyowasilishwa bungeni, unatokaje nje ukichangia kuhusu Barrick? (CCM) Wawe wavumilivu hata katika mambo ambayo hawataki kuyasikia,” alisema.

Naye mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Seriki za Mitaa (LAAC), Vedustus Ngombale alisema wabunge kuzungumza hoja zilizo nje ya mjadala ni jambo la kawaida kwa kuwa ni wanasiasa, lakini anayeongoza Bunge anapaswa kuwaelekeza.

Alisema kanuni zinamruhusu Spika, Naibu Spika au mwenyekiti aliyeko mbele kwa wakati huo kuwa makini kwa kujua kitu gani kimewasilishwa na kinapaswa kuchangiwa wakati huo.

“Wabunge ni wanasiasa, ukimuachia nafasi bila kumwelekeza, lazima ataingiza mambo yake tu,” alisema Ngombale.

Wadau nao wafunguka

Dk Onesmo Kyauke, mwanasheria na mchambuzi wa masuala ya kisiasa alisema kwa kawaida mabunge yote ya mfumo wa vyama vingi yanakutana na changamoto ya aina hiyo, akitoa mfano wa Bunge la Senate la Marekani.

“Kikubwa ninachoona ni kutafuta kick tu za kisiasa. Lakini tatizo jingine ni uwezo wa mbunge mmoja mmoja kukosa maarifa ya kujenga hoja kuhusu mjadala. Kwa sababu kama una data za kutosha kuhusu hoja iliyopo mezani, itakusaidia tu kupata umaarufu au kukuza uhai wa chama,” alisema Kyauke.

Jana vijembe hivyo vilianza wakati mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche alipokuwa akitumia nafsi ya p;ili ya uwingi kuisema CCM kama chama kilichoshika Serikali badala ya kuikosoa Serikali kama wanavyofanya wakati wa mijadala mikali ya kufichua ufisadi wanapoungana kuwa kitu kimoja.

Heshe jana alitumia fursa ya kujadili mkataba wa kampuni ya uchimbaji madini ya Barrick na Serikali kuhusu kipengele kinachozungumzia usuluhishi, ambacho awali sheria ilitaka suala hilo lifanyike ndani ya nchi lakini baadaye ikabadilishwa.

Alisema CCM huwa wanawazungumzia wapinzani kuwa ni vibaraka wa mabeberu kila wanapokosoa masuala hayo, akisema wanaofuata maelekezo ya mabeberu ni wao kwa kuwa wamekubali kubadili sheria kufuata utashi wao.

Alikuwa akisema hayo huku wabunge wanaoonekana kuwa wa CCM wakisimama kutaka kutoa taarifa au kuomba mwongozo.

Pia alizungumzia suala la upatikanaji wa nishati akisema baada ya miaka 50 ya uhuru mi Watanzania milioni 2.8 tu waliounganishiwa nishati hiyo.

“Huu ni mwaka wa uchaguzi. Wateja milioni 2.8 tu wameunganishiwa umeme. (CCM) Mnafanya kama kitu cha anasa. Gharama za kuunganisha umeme ni za nini? Ukimuunganishia si atakulipa bili kila mwezi?” alihoji.

Alisema wanapaswa kuondoka madarakani na kupisha watu ambao watawaunganishia watu wengi umeme bure na kwa kipindi kifupi.

Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani alisema Heche hawezi kulinganisha idadi ya watu waliounganishiwa umeme na ya watu nchini.

Alisema upatikanaji wa umeme mjini umeongezeka kutoka asilimia 92.2 mwaka 2015 hadi asilimia 97 mwaka 2019, vijijini asilimia 49.5 hadi asilimia 72.5.

Ndugai aliwakumbusha wabunge kuwa ni vizuri kujua taratibu za kibunge kwa sababu aliyetoa hoja hiyo ya kamati ni mwenyekiti wa kamati na si waziri.

“Kwani mwenyekiti ndiye aliyeingia huu mkataba au atakuja kujibu, hii ni hoja ya mwenyekiti wa kamati. Hoja zetu tunaelekeza kwa mwenyekiti na tunashauri kamati, Bunge na Serikali,” alisema Ndugai.

Hata hivyo, Heche alisema anajua mawaziri wanapewa nafasi ya kujibu masuala hayo kama ilivyofanyika katika taarifa nyingine za kamati za Bunge.

Kuhusu mitambo ya kuyeyusha michanga iliyosalia na dhahabu, yaani smelter, Heche alisema sheria ilitungwa kuwa kuanzia sasa madini ghafi hayatasafirishwa nje na kuhoji wapi smelter imejengwa.

Lakini Waziri wa Madini, Dotto Biteko alisema Heche anafahamu kila kinachoendelea kwenye ujenzi wa smelter.

“Kujenga Smelter, si kama kujenga kibanda, ni teknolojia kubwa. Wataalamu wote walisema kujenga smelter kunachukua miezi 24, tumeshatoa leseni kwa ajili ujenzi huo,” alisema.

Hata hivyo, Heche alisema sasa wanaelekea miezi 26 lakini hakuna smelter. “Kwanini mnasema makontena yasafirishwe? Kifungu 11 kinasema wazi kabisa ni marufuku kusafirisha nje ya nchi madini ghafi,” alisema.

Kauli hiyo ilimuibua Biteko ambaye alisema hafurahi kujibizana kwa sababu kifungu namba 59 kimetoa fursa kwa waziri mhusika kutengeneza, kusafirisha madini yaliyosafishwa kwa kiasi fulani kwa muda. Hata hivyo, Ndugai alisema neno upinzani lina shida na kwamba, wafikie mahali wakawa na neno ushindani.

Alisema heche ni mjumbe wa kamati hiyo lakini anapotosha wabunge ambao hawako kwenye kamati hiyo.

Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy alisimama kumtetea.

“Kuna wabunge hawajamaliza kutembelea vijiji vyao, lakini waziri na naibu wake wametembea kila jimbo kila kona. Wako wabunge wanaishia Dodoma na Dar es salaam. Mheshimiwa aliyetoka kuzungumza hahudhurii vikao kwa sababu kila siku yuko kwenye kesi dar es Salaam,” alisema.