Sido yamwaga Sh43 milioni kwa wafanyabiashara

Saturday February 22 2020

By Mwanja Ibadi, Mwananchi [email protected]

Lindi. Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Tanzania (Sido) limewapatia wafanyabiashara wadogo mkopo wa Sh43 milioni kwa ajili ya kuboresha mitaji yao.

 

Akizungumza  jana Ijumaa Februari 21, 2020 meneja wa Sido Mkoa wa Lindi, Kasisi Mwita amesema  shirika linatoa mikopo  kwa wananchi kutoka mfuko wa Taifa wa kuendeleza wafanyabiashara (NEDF).

 

Mwita amesema hadi Desemba 31,  2019  mikopo 1,388 ya Sh1.9 bilioni imetolewa ambayo ni wastani wa Sh1.4 milioni kwa kila mtu.

 

Advertisement

Amebainisha kuwa vikundi 48 vimepata mikopo,  wanawake 534 wanaume 546  na kwamba waliopewa wanarejesha vizuri na kusaidia kupanda kwa ukopeshaji , “kwani kwa kipindi cha miaka minne Sh895.9 milioni zimewafikia wafanyabiashara 414.

 

Mkuu wa Wilaya Lindi,  Shaibu Ndemanga amewataka wafanyabiashara  hao kutumia mikopo hiyo katika shughuli walizopanga kuzifanya ili waweze kujikwamua kiuchumi.

 

Amewataka wafanyabiashara kuwa wabunifu ili waweze kurejesha mikopo yao kwa wakati.

 

Baadhi ya wafanyabiashara hao, Amina Halfani  na Mustafa Hasani  wameshukuru Sido kwa kuwapa mikopo yenye riba nafuu itakayosaidia kuinua mtaji wao.

 

Advertisement