Sifa mgombea uchaguzi Serikali za mitaa kuwa kada wa CCM yasimamisha bunge dakika tatu

Kauli ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa ilivyofanya wabunge wa chama tawala (CCM) na wapinzani kushindwa kujizuia hisia zao na kuanza kupiga kelele huku wengine wakishangi wakati Bajeti Kuu ya Selikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020, ilipokuwa ikiwasilishwa bungeni jijini Dodoima leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Sifa za wagombea wa uchaguzi huo utakaofanyika Oktoba 2019 zimetajwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango wakati akiwasilisha bajeti ya Serikali Kuu mwaka 2019/2020 aliposisitiza kuwa amepewa baraka ya kueleza hayo na Rais John Magufuli. 

Dodoma.  Wabunge wa vyama vya upinzani leo Alhamisi Juni 13, 2019 bungeni jijini Dodoma wamesimama kwa takribani dakika tatu huku wakizomea na kupiga meza baada ya kuelezwa kuwa moja ya sifa ya wagombea katika uchaguzi wa Serikali za mitaa ni kuwa wanachama wa CCM.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango wakati akiwasilisha bajeti ya Serikali mwaka  2019/2020 ambayo ni Sh33.1 trilioni.

Wakati akihitimisha kuwasilisha kusoma bajeti hiyo, Dk Mpango aligusia uchaguzi huo utakaofanyika Oktoba 2019 kuwa ni kuchagua mtu anayetoka CCM.

"Sifa ya 10  awe anatoka ndani ya chama cha siasa kinachotetea maslahi na haki za wanyonge na chama hicho ni CCM, " amesema Dk Mpango.

Baada ya kauli hiyo ambayo Dk Mpango aliirudia mara tatu, wabunge wa upinzani walisimama huku wakipiga meza zao na kuimba "CCM, CCM, CCM. "

Wakati wapinzani wakiwa wamesimama,  wabunge wenzao wa CCM nao walisimama na kusababisha Dk Mpango kusimama kuwasilisha bajeti hiyo kwa dakika tatu.

Spika Job Ndugai na kaimu mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,  Joseph Selasini walitumia nguvu ya ziada kuwatuliza wabunge wa pande zote mbili,  kumpa nafasi Dk Mpango kumalizia hotuba yake.

Dk Mpango alipopewa nafasi ya kuendelea kuwasilisha amesema alichokisema kina baraka ya Rais John Magufuli.