Sifa za wahudumu ATCL zawekwa wazi, mvuto si kigezo

Muktasari:

Mkurugenzi Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) Ladislaus Matindi amesema sifa ya mhudumu wa ndege ni elimu na vigezo vinavyokubalika kimataifa na kitaifa.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) Ladislaus Matindi amesema sifa ya mhudumu wa ndege ni elimu na vigezo vinavyokubalika kimataifa na kitaifa.

Amesema mvuto kwa wahudumu wa ndege za shirika hilo sio lazima, haupo kwenye viwango na kanuni, “ingekuwa sheria zetu zinataka wanaotembea kwa maringo tungewachukua lakini na huduma nazo zingetolewa kwa maringo.”

Ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Novemba 9, 2019 katika mkutano wake na waandishi wa habari akitoa ufafanuzi wa kauli ya mbunge wa Kigoma Kusini (CCM), Husna Mwilima ambaye siku mbili zilizopita bungeni mjini Dodoma alisema wahudumu wa shirika hilo hawana mvuto kwa wateja.

Amesema lengo la mkutano huo na wanahabari ni kutoa elimu kwa wananchi wasiokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu sifa za wahudumu wa ndege.

"Kusema kuwa wahudumu ni wafupi si kweli. Waliopo wana urefu wa futi  5.2 na wanaweza kuyafikia maeneo yote (ndani ya ndege), hilo la ufupi sijui limetoka wapi. Hata kusema ni watu wazima sio kweli wanaanzia umri wa miaka 18 hadi 48.”

"Siyo kama hatutaki kupokea maoni ya wadau lakini yanapotolewa kinyume tunapaswa kutoa elimu ili kuondoa mkanganyiko," amesema Matindi, akibainisha kuwa kinachotakiwa ni huduma stahiki.

Amesema vigezo vinavyotajwa kwa sasa vinapaswa kutajwa katika tasnia nyingine za ulimbwende.