VIDEO: Simbachawene aagiza mkandarasi kuwekwa ndani

Mkandarasi wa Kampuni ya Nangonga Ltd Mohammed Nangonga (tsheti nyekundu) akiwa chini ya ulinzi baada ya agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi George Simbachawene la kutaka akamatwe kwa kutengeneza barabara bila kuweka alama katika eneo la Ihumwa jijini Dodoma. Nazael Mkiramweni

Muktasari:

Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania,  George Simbachawene ameagiza Mohamed Nangonga ambaye ni mhandisi wa kampuni ya Nangonga Ltd kukamatwa kwa madai ya uzembe  wa kutoweka alama za barabarani na kusababisha vifo vya watu watatu.

Dodoma. Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania,  George Simbachawene ameagiza Mohamed Nangonga ambaye ni mhandisi wa kampuni ya Nangonga Ltd kukamatwa kwa madai ya uzembe  wa kutoweka alama za barabarani na kusababisha vifo vya watu watatu.

Mkandarasi  huyo anasimamia kuweka viraka katika eneo la Ihumwa jijini Dodoma barabara ya Dodoma- Morogoro.

Akizungumza leo Jumatano Aprili 15, 2020, Simbachawene amesema kampuni hiyo imechimba mashimo katika eneo hilo na kuyaacha muda mrefu bila kuweka alama.

Amesema uwepo kwa mashimo hayo umesababisha ajali mbili na watu watatu kupoteza maisha.

"Wewe ni rafiki yangu lakini katika hili ni lazima uwajibike, unachimba mashimo barabarani huweki alama ili wenye magari wajue kuna matengenezo yanayofanyika.”

"Nilipita juzi hapa nikaona haya mashimo nikasema yanaweza kukaa muda mrefu bila kutengenezwa  matokeo yake sasa kunatokea vifo huu ni uzembe, naagiza mkandarasi huyu akamatwe pamoja na vibarua wake,” amesema Simbachawene.

Baada ya agizo la waziri mkandarasi huyo aliwekwa chini ya ulinzi na askari polisi waliokuwepo eneo la tukio.