Simbachawene achukua nafasi ya Lugola, Zungu awa waziri

Muktasari:

Rais John Magufuli amemteua mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Azzan Zungu kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) huku aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, George Simbachawene akiteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amemteua mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Azzan Zungu kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) huku aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, George Simbachawene akiteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.

Simbachawene anachukua nafasi ya Kangi Lugola ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Hayo yameelezwa leo jioni Alhamisi Januari 23, 2020 na katibu mkuu kiongozi, Balozi John Kijazi.

Mabadiliko hayo madogo ya baraza la mawaziri yamefanyika baada ya leo asubuhi katika hafla ya uzinduzi wa nyumba za askari wa Jeshi la Magereza zilizopo Ukonga, Dar es Salaam, Rais Magufuli kueleza kutoridhishwa na utendaji kazi wa Lugola na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye ambaye naye uteuzi wake umetenguliwa, huku ikielezwa nafasi yake itajazwa baadaye.

Katika uteuzi huo, Rais Magufuli amemteua aliyekuwa katibu mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Jacob Kingu kuwa balozi.

Katika hafla ya uzinduzi wa nyumba hizo, Magufuli alisema Meja Jenerali Kingu aliandika barua ya kujiuzulu na alimkubalia,  kueleza kuwa amemheshimu kwa uamuzi wake huo.

“Leo Rais Magufuli amemteua Zungu kuwa Waziri anayeshughulikia muungano na mazingira na kumhamisha Simbachawene kwenda Wizara ya Mambo ya Ndani  kuchukua nafasi ya Lugola ambaye uteuzi wake umetenguliwa,” amesema Balozi Kijazi.

Amesema Rais Magufuli pia amefanya uteuzi wa mabalozi watatu watakaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali baada ya waliokuwepo kumaliza muda wao, kufikisha umri wa kustaafu.

“Amemteua Meja Jenerali Kingu ambaye alikuwa katibu mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani kabla ya kujiuzulu jana Januari 22, 2020.”

“Amemteua Dk Steven Simbachawene kutoka ofisi ya rais Ikulu na kamishna Jenerali Faustine Kasike ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, nafasi ya Kasike itajazwa baadaye. Vituo vya kazi vya mabalozi hawa watatu vitatangazwa baadaye,” amesema balozi Kijazi.

Balozi Kijazi amesema Rais Magufuli amewaongezea muda mabalozi saba wa Tanzania, akiwemo Asha Rose Migiro ambaye ni balozi wa Tanzania nchini Uingereza.