VIDEO: Simulizi wanaojifungua chumba cha wagonjwa wanaosafishwa vidonda

Tuesday October 22 2019

zahanati ya Lugulu ,mwananchi habari gazeti, Wilaya ya Same,Jerna Basili

 

By Janeth Joseph, Mwananchi [email protected]

Same. Kukosekana wodi ya wajawazito katika zahanati ya Lugulu iliyopo Wilaya ya Same, kumesababisha wanaotaka kujifungua watumie chumba kimoja na wagonjwa wanaosafishwa vidonda.

Wakizungumza na Mwananchi, wakazi wa Kijiji cha Lugulu ilipo zahanati hiyo wamedai kuwa baada ya kujifungua wanawake walikuwa wakibebeshwa uchafu kutokana na kukosekana shimo maalumu la kutupia taka hizo.

Jerna Basili, mkazi wa kijiji hicho alisema kitendo cha wao kuchanganywa chumba kimoja na wagonjwa wengine ni udhalilishaji usiovumilika.

“Hebu fikiria mama anajifungua sehemu ambayo kuna wagonjwa wengine wanasafishwa vidonda. Licha ya kumdhalilisha mama, pia tunamuweka katika mazingira hatarishi mtoto anayezaliwa,” alisema.

Jerna alisema awali wanawake hao walikuwa wakibebeshwa uchafu, lakini hivi karibuni uongozi wa zahanati hiyo umeamuru uchafu huo utupwe chooni.

“Hebu fikiria lile kondo linatupwa kwenye choo cha shimo, hicho choo kitaingilika kweli kama vinachanganyika huko, na usalama wa afya kwa watumiaji wengine ukoje?” Alihoji Jerna.

Advertisement

Aliwaomba viongozi kuanzia ngazi ya wilaya hadi mkoa, kutatua changamoto hiyo kwa sababu wakazi wa vijiji vitatu wanaitegemea zahanati hiyo.

Akizungumzia changamoto hizo, mhudumu wa zahanati hiyo Vailet Mushi alikiri kuwa zahanati hiyo ina changamoto ya vyumba na kwamba mara nyingi wanalazimika kutoa huduma zaidi ya moja kwenye chumba kimoja.

“Tuna upungufu wa vyumba, chumba kimoja kinatumika kutoa huduma ya aina zaidi ya moja. Kwa mfano chumba cha kuzalisha akina mama tunapatumia pia kwa wagonjwa wenye vidonda wanaokuja kuvisafisha na kuchomea sindano, changamoto ni kubwa,” alisema Vailet.

Alisema licha ya kukosekana kwa wodi ya wazazi, zahanati hiyo inakabiliwa na ukosefu wa shimo maalumu la kutupia uchafu baada ya mzazi kujifungua hali inayowalazimu kutupa taka hizo kwenye choo cha shimo.

“Licha ya akina mama kujifungulia kwenye zahanati hiyo hatuna shimo la kutupia taka baada ya wao kujifungua, hivyo tunalazimika kutupa chooni na kisheria hii haifai, kondo la nyuma kutupwa chooni ni tatizo na linatupa wakati mgumu,” alisema Vailet.

Alifafanua kuwa awali kabla ya kupata wazo la kutupia taka hizo chooni walikuwa wakiwabebesha wazazi taka hizo kwenye mifuko ili wakatupe majumbani mwao.

“Kipindi cha nyuma wazazi walikuwa wakiondoka na kondo la nyuma baada ya kujifungua ili wakatupe nyumbani wakati kiafya hairuhusiwi, ni kero kwetu sisi wahudumu na kwa jamii maana utupaji wa kondo la nyuma (placenta) wengi hawajui, wanatupa ovyo na inakuwa kama uchafu,” alisema Vailet.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Credianus Mgimba alisema kimsingi hali hiyo haipaswi kuwepo na kwamba ni jukumu la serikali ya kijiji kuhakikisha wanashirikiana kwa pamoja kuchimba shimo kwa ajili ya taka hizo na shughuli nyingine.

Mbunge wa jimbo hilo, Naghenjwa Kaboyoka alisema kwamba amekuwa akijitahidi kadri iwezekanavyo kupiga kelele serikalini kupatiwa fedha kwa ajili ya kusaidia jengo la wodi za akina mama, lakini hajapewa fedha hizo.

“Kwa kweli ni fedheha kubwa, cha kushangaza Tarafa ya Gonja haina kituo cha afya hata kimoja badala yake tarafa yote inategemea vituo vya afya vya kanisa la KKKT na RC,” alisema Kaboyoka.


Advertisement