JELA PANAPOKUWA KIMBILIO: Simulizi ya mfungwa wa Mbeya aliyesamehewa na Rais Magufuli

Busokelo. Merad Abraham (58), aliyeachiwa kwa msamaha wa Rais John Magufuli katika maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika na kugoma kutoka katika gereza la Ruanda mjini Mbeya, anaishi maisha ya hofu na hataki kukaa na watu.

Hayo yameelezwa na Abdul Mwaitege ambaye ni mjomba wa Merad katika mahojiano na Mwananchi nyumbani kwake kijiji cha Kandete-Mwakaleli wilayani Rungwe.

Hata hivyo, majirani wa Merad wanasema kuwa mtu huyo anahitaji msaada wa wanasaikilojia kumrudisha katika hali ya kawaida.

Merad alifungwa mwaka 2000 baada ya kukutwa na hatia ya kubaka.

Mfungwa huyo ni kati ya wafungwa 5,533 walioachiwa kwa msamaha wa Rais Magufuli Jumatatu iliyopita, lakini aligoma akidai hana pa kwenda kabla ya kuamua kujijeruhi katika paji la uso.

Hata hivyo, askari magereza walimkabidhi kwa ndugu zake baada ya kumdanganya kuwa anahamishiwa gereza la Ukonga, Dar es Salaam alikokuwa akiomba kurudishwa.

Hata hivyo siku Merad anaachiwa gerezani mkuu wa magereza Mkoa wa Mbeya, Mathias Mkama alisema hakuwa na akili sawasawa na huenda ni kutokana na kukaa gerezani muda mrefu.

“Lakini nithibitishe tu kwamba alitoka gerezani vizuri tu na ndugu zake walikuja gerezani na kumchukua,” anasema Mkama.

Alivyofungwa

Akizungumzia kifungo cha ndugu yake huyo, Mwaitege alisema wakati akiishi Dar es Salaam alipewa taarifa kwamba Merad ana kesi ya kubaka na amefungwa gereza la Rungwe.

Alisema wakati kesi ikiendelea mahakamani, aliyedaiwa kubakwa alipimwa na kubainika hakubakwa lakini kesi iliendelea na ndugu yake kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.

“Basi akakaa gereza la Rungwe na baadaye tukaambiwa ndugu yetu amehamishiwa Gereza Kuu la Ruanda jijini Mbeya. Baada ya hapo mama yake aliendelea kuhangaika lakini muda mwingi akawa anapigwa chenga.”

“Bibi yangu ambaye ni mama yake Abraham alianza kutumia gharama nyingi za nauli kwenda na kurudi hadi jijini Mbeya kufuatilia suala la mtoto wake bila mafanikio,” alisema akibainisha jinsi mama huyo alivyouza viwanja kupata fedha kufuatilia kesi ya mwanaye.

Alisema baada ya baba yake Abraham kufariki ambaye alikuwa akifuatilia kesi hiyo pamoja na mkewe, mama yake mdogo Merad alianza kufuatilia kesi hiyo lakini naye alifariki dunia.

Alisema baadaye askari magereza mmoja ambaye hamkumbuki jina aliwapa taarifa kuwa Merad amehamishiwa gereza la Ukonga.

Mwaitege alisema baadaye Merad alianza kutokuwa sawa kisaikolojia kutokana na kuanza kueleza kuwa hana ndugu.

Alisema wakati wakianza kumfuatilia katika gereza la Ukonga wakapata taarifa kuwa amehamishiwa gereza la Ruanda na ndipo walipoanza kumtembelea.

Alibainisha kuwa alipokuwa gerezani Mbeya ndugu zake walisikia amepata msamaha wa Rais na walipokwenda kumchukua aliwagomea hivyo akabaki gerezani.

“Ila huu msamaha wa sasa tulipomsikiliza Rais tukafuatilia kuona kama amepata na yeye tena. Bahati nzuri tukaona hata mtandaoni kwamba amepata msamaha huo lakini hataki kutoka gerezani hapo,” alisema Mwaitege.

Ugumu kumtoa gerezani

Alisema walipokwenda kumchukua iliwachukua muda mrefu kuondoka naye kwa kuwa aligoma, walisaidiwa na maofisa wa Magereza.

“Siku ya kwanza alichukua jiwe na kujibonda kwenye paji la uso, ikawalazimu askari magereza watusaidie. Walimdanganya kuwa wanampeleka gereza la Ukonga ndipo akakubali kuingia kwenye gari.”

“(Merad) alipoelezwa hivyo alianza kujiandaa kufungasha vitu vyake lakini hata hivyo askari walilazimika kumfunga pingu akiwa kwenye gari hadi hapa nyumbani,” alisema Mwaitege.

Alisema walipofika nyumbani shughuli ikawa kwenye kumshusha, “alisumbua sana baada ya kuona huku si kule alikoambiwa anapelekwa (Ukonga), lakini tunashukuru askari walitusaidia na wakamfungua pingu na kumuingiza ndani.”

Alisema tangu siku hiyo alipofikishwa nyumbani kwao, hakuwa tayari kuzungumza na mtu yeyote wala kusalimiana kwa kushikana mikono.

Alisema kwa sasa Abraham hataki msongamano wa watu wengi, kwani watu wakikusanyika nyumbani kwao anaondoka na kwenda kujifungia ndani.

Kumbukumbu zinamjia

Mwaitege alisema akianza kuzungumza pekee yake, anawakumbuka ndugu zake aliowaacha kwa kuwataja majina lakini wanamuambia walishafariki akiwemo mama na baba yake mzazi.

“Hadi sasa anamzungumzia sana yule mzee aliyempa kesi kwamba amembaka mtoto wake anaitwa (anataja jina), huyu ndiye anamzungumzia sana akisema huyo ndiye aliyemsingizia na ndiye aliyemharibia maisha,” alisema Mwaitege.

Alisema kadri siku zinavyokwenda akili inamjia na kuanza kukubali kuzungumza machache na baadhi ya watu wanaomtembelea nyumbani hapo.

“Hapa anayezungumza naye sana ni mtoto huyo hapo, kama anahitaji chakula au maji basi anamwambia huyo binti’, alisema akimuonyesha binti huyo.