Siri ya Graiyaki na Twiboki shule pacha kuongoza darasa la saba

Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde 

Serengeti. Ni shule za mmiliki mmoja na zote zipo wilaya moja ya Serengeti mkoani Mara. Ndizo shule zilizofanya vizuri zaidi katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba yaliyotangazwa Jumanne 15, 2019 na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta).

Graiyaki ndiyo iliyoshika nafasi ya kwanza ikifuatiwa na shule pacha ya Twibhoki iliyoshika nafasi ya pili katika orodha ya shule 10 bora kitaifa.

“Sio mara ya kwanza kuongoza kitaifa. Tumefanya hivyo mwaka 2010, kiwilaya na kimkoa tangu mwaka huohuo hadi sasa. Miaka ya katikati kitaifa tumekuwa tukicheza kwenye kumi bora, na hii ni kwa sababu ya kuheshimu mpango kazi tunaojiwekea,”anasema meneja wa shule hizo, Grace Godfrey.

Kinachovutia ni kuwa hii ni mara ya kwanza kwa Graiyaki kutoa wahitimu wa darasa la saba, na katika hilo Grace anasema siri ya shule hiyo kufanya vizuri ni kuwatumia walimu waliotoka Twibhoki yenye historia ya ufaulu sambamba na kuwapa wanafunzi mitihani ya mara kwa mara.

“Walimu wanajua nataka nini sipendi nini kwenye kazi,binafsi tunatumia gharama kubwa kuchapisha mitihani maana kila wiki ni mtihani hasa kwa darasa la saba, ndiyo maana mitihani kwao wanaona kitu cha kawaida,”alisema.

“Hapa ushirikiano ni silaha kubwa na kila mwalimu anaguswa anapoona mtoto fulani hajamudu somo fulani. Wanakaa pamoja na kuelekeza nguvu kuhakikisha wamemweka sawa, maana kilichowaleta hapa ni kusoma na walimu kuwafundisha hakuna biashara zaidi ya hiyo.’’

Siri ya Graiyaki

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Graiyaki, Sonda Majaliwa anasema maandalizi yao yalilenga kuwawezesha watoto kushinda.

“Kwanza ni kuwaondoa hofu waone mtihani ni jambo la kawaida, ndiyo maana darasa la saba kila mwezi wanafanya mitihani na inawajenga kujiamini,”alisema.

Shule hiyo imetoa wahitimu watano katika orodha ya wanafunzi 10 bora kitaifa. Majaliwa anasifu mshikamano wanaoupata walimu kutoka kwa viongozi wa shule.

“Meneja anapata wakati wa kuwasikiliza wanataka nini, hawataki nini,’’alisema.

Siri ya Twibhoki

Mkuu wa Shule ya Msingi Twibhoki, Samson Nhandi alisema “tumewafundisha watoto kutokufuta wanapokuwa kwenye mitihani, kama amekosea anatakiwa kuacha hivyo sisi watoto wamezoea hivyo ndiyo maana kwenye mitihani wanakuwa hawana wasiwasi.’’

Alisema kwa wiki wanafanya mitihani na kuwapa motisha wale wanaofanya vizuri, jambo alilosema linawasaidia kukuza taaluma.

Alisema shule yao haina utoro wowote kwa kuwa wazazi wanajua wajibu wao kwa kuwapeleka watoto shule kwa wakati.

“Tunafundisha masomo ya kiada na ziada ili kuwaongezea maarifa mengi na hiyo ni silaha kubwa ya ushindi wetu wa mara kwa mara kwa mitihani ya kiwilaya, kimkoa na kitaifa,”alisema.

Katika matokeo ya mwaka huu, shule hiyo imekuwa ya pili kitaifa huku ikitoa wanafunzi wawili katika orodha ya wanafunzi 10 bora.