RIPOTI MAALUMU: Siri ya Wahadzabe kuvuta bangi-3

Sunday September 22 2019

 

By Florence Majani, Mwananchi

Naingia katika nyumba ya Lameck Lucas, maarufu kama Fama, ni saa saba mchana.

Fama na familia yake wanaishi katikati ya pori la Domanga, ilipo jamii ya Wahadzabe ambayo bado inatunza mila zake.

Nyumba hii yenye nyasi tupu, nje imezungukwa na miti kadhaa ambayo inatengeneza kivuli kizuri kwa familia hii.

Fama yupo na mke wake, Elinoli Lameck na wajukuu zake 12.

Ninapoingia katika familia hii, namkuta Elinoli akitengeneza chakula cha mchana cha siku hiyo, ambacho ni matunda aina ya Imbilibi.

Elinoli, anatayarisha matunda haya kwa kuyachanganya na maji ili kupata juisi.

Advertisement

Asubuhi, yeye na wajukuu zake walipata kifungua kinywa cha matunda ya ubuyu.

“Hatuna shaka juu ya milo hii, ndiyo iliyotukuza, hadi leo nina watoto sita na wajukuu 12,” anasema.

Wakati tunaendelea na mazungumzo haya, mume wa Elinoli, Fama anavuta kiko chake na kwa haraka naitambua harufu ya moshi unaotoka ndani ya kiko hicho kuwa ni wa bangi.

Namuuliza Fama ni kipi anachovuta na ananiambia ni bangi. Ninamuuliza kwa nini anavuta bangi hiyo tena hadharani?

Anashangaa na kusema haoni ajabu ya yeye kuvuta bangi kwani ni sehemu ya mila zao.

“Sisi tunavuta bangi kama sehemu ya mila, huwezi kwenda kuzungumza na mizimu kama hujavuta bangi,” anasema.

Fama anasema Wahadzabe hutambikia mizimu yao eneo la Dundubi ambako kuna jiwe kubwa linaloaminiwa kuwa ndimo mizimu ilipo.

“Kabla ya kwenda ni lazima tusali sana kuwaomba mizimu waturuhusu kwenda, wazee ndio wanaokwenda kuzungumza na mizimu, si kila mtu,” anasema.

Fama anasema wazee huona dalili iwapo mizimu imewaruhusu kwenda au imekasirika.

“Kama mizimu imeruhusu sisi kwenda, tunaenda na kabla hatujapanda kwenye jiwe kuzungumza nayo, tunawaomba watupe ruhusa. Ili kupata ruhusa hiyo, pamoja na mambo mengine, ni lazima tuwe tumevuta bangi,” anasema.

Anasema pamoja na bangi, pia ni lazima kutafuna mti uitwao, Keragumukwao ili kupata baraka za mizimu hiyo.

Anasema mara baada ya kuruhusiwa hupanda katika mlima huo mkubwa ambao juu una mawe mengine matatu yaliyojipanga kama mafiga na kuanza kuzungumza na mizimu.

“Kikubwa tunachoiomba mizimu ni usalama wetu, vyakula vyetu na kuwaombea wanyama ambao ni sehemu yetu,” anasema.

Akizungumzia zaidi kuhusu matumizi ya bangi kwa jamii hiyo, Fama anasema bangi inawawezesha kufanya kazi kwa nguvu bila kuchoka.

“Nikivuta hapa, ninaweza kuwinda na kufanya kazi zote mchana kutwa bila kuchoka,” anasema.

Anasema si wanaume tu wanaovuta bangi bali hata wanawake kwani ni sehemu ya mila za Wahadzabe.

Meneja mradi wa utunzaji wa mazingira wa Carbon Tanzania, Isaack Magombe anasema bangi iliruhusiwa kwa jamii ya Wahadzabe kutokana na aina ya maisha yao.

“Ninachokumbuka ni kuwa, bangi ni halali, ila sijui kama wananunua wapi au wanalima humu humu kwenye makazi yao,” anasema.

Elinoli, mke wa Fama alizungumzia mila nyingine za Wahadzabe ikiwamo vyakula na majukumu.

Anasema mama ndiye mtafutaji wa chakula cha familia ambacho ni matunda na mizizi.

“Hata hii leo huu ubuyu na hizi Imbilibi nilikwenda kutafuta mimi. Nilisindikizwa na baadhi ya wajukuu zangu,” anasema.

Anasema kunapokucha, mwanamke hujipanga kutafuta chakula kwa ajili ya familia ingawa na baba au wanaume nao hutoka kwenda kuwinda na kuangalia kama kuna asali.

Elinoli anasema katika jamii za Wahadzabe hakuna anayefanya kazi peke yake au familia moja kutafuta chakula chake peke yake bali eneo zima (nyumba tatu au nne) hushirikiana.

“Kwa mfano, nyumba tatu au nne zinazokaa karibu, huondoka kwa pamoja kutafuta matunda na mizizi au kama ni kuwinda,” anasema.

Anasema chakula kinachopatikana huliwa kwa pamoja hata kama ni kidogo hugawanywa sawa kwa wote na kwa kuzingatia umri.

“Lakini kwa kipindi hiki, wanaume hawawindi kwa sababu kuna vipindi ambavyo tunapumzika kuwinda,” anasema.

Fama anatoa ufafanuzi kuwa Wahadzabe wamejipangia kutenga vipindi vya kuwinda na kutokuwinda ili kutoa nafasi kwa wanyama kuzaliana.

“Ndiyo maana unaona miaka inaenda na wanyama wapo, lakini wanaomaliza wanyama ni majangili,” anasema.

Elinoli anasema kwa bahati mbaya, tumefika katika kipindi ambacho wamesimama kuwinda la sivyo tungekula kitoweo cha nyama ya nyani.

“Hii ni nyama muhimu kwetu, hata mahari kubwa ni dume la nyani,” anasema.

Fama huku akitengeneza mishale yake anafafanua kuwa kitoweo kikubwa kwa Wahadzabe ni nyama ya nyani, lakini pia wanakula pofu, swala, impala na khanga.

Akizungumzia zaidi mila zao, Elinoli anasema mwanamke ana mamlaka makubwa katika jamii za Wahadzabe.

Anasema kwa mfano, hata katika ndoa, mwanamke wa familia moja ndiye anayekwenda katika familia nyingine kuposa.

“Mimi mwanamke kama nina kijana wangu, nitakwenda kwenye familia yenye msichana mzuri kwa ajili ya kijana wangu, baadaye ndipo tunawashirikisha wanaume,” anasema.

Anasema hata ujenzi wa nyumba mara nyingi hufanywa na mwanamke.

Kuhusu masuala ya uzazi, Elinoli anasema aghalabu mwanamke wa Kihadzabe hajifungui hospitali bali husaidiwa na mkunga wa jadi.

“Hata kama watakuja madaktari hapa na wakae hapa, sisi hatuwezi kuzalia hospitali, Mhadzabe anazaa nyumbani na hatujawahi kusikia mtu kafariki wakati akijifungua,” anasema.

Anasema zipo dawa za asili wanazokunywa wanawake kabla na baada ya kujifungua ambazo zinawasaidia wanawake hao.

“Lakini si mizizi pekee, sisi tumerithishwa na wazazi namna sahihi ya kumsaidia mwanamke kujifungua salama na mtoto kuwa salama,” anasema.

Hata hivyo fedha zinazoletwa kupitia mradi wa Carbon Tanzania, huwawezesha madaktari kutembelea wakazi wa jamii ya Wahadzabe kila mwezi ili kuwapima afya.

Marc Baker, Mwanzilishi wa kampuni ya Carbon Tanzania, anasema kliniki hizo hupima na kutibu magonjwa kama kifua kikuu, macho na magonjwa mengine.

Advertisement