VIDEO: Sirro azungumzia vurugu Zanzibar

Muktasari:

IGP Simon Sirro amesema Jeshi la Polisi limejipanga kupambana na wanaovunja amani kuelekea uchaguzi mkuu kesho Oktoba 28.

Dar es Salaam. Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro amesema kuna watu 42 waliokamatwa kisiwani Pemba wakidaiwa kuwashambulia polisi waliokuwa wakisambaza masanduku ya kura jana.

IGP Sirro amesema hayo leo Oktoba 27 jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu taarifa za vikundi vya watu wanaotaka kufanya vurugu.

"Kama kule Zanzibar, wakati askari wanasambaza masanduku ya kupigia kura, kuna vijana walianza kurusha mawe na wameshulikiwa. Wapo karibu 42. Mpaka sasa hakuna kifo chochote," amesema IGP Sirro.

Hali visiwani inaonekana kuwa ya vurugu, huku milio ya mabomu ya machozi ikisikika sehemu kadhaa mapema leo, huku Jeshi la Polisi Zanzibar likisema kuwa limelazimika kutumia mabomu kutawanya watu walionekana kutaka kuvunja amani.

Zanzibar, inayoundwa na visiwa vikuu vya Unguja na Pemba ina ushindani mkali wa kisiasa, ambao hujidhihirisha wakati wa uchaguzi, hali mbaya zaidi ikionekana baada ya uchaguzi wa mwaka 2000 wakati vurugu kubwa zilipoibuka na kusababisha watu takriban 20 kupoteza maisha na wengine kadhaa kukimbilia Shimoni nchini Kenya.

Kuhusu upigaji kura, Siro alisema na a kuwa jeshi lake limejipanga vizuri kukabiliana na hali yoyote ya uvunjifu wa amani.

"Tumejipanga vizuri kuhakikisha hakuna uvunjifu wa amani. Kesho asubuhi kama ni mmoja wa wanaokwenda kupiga kura, nenda ukapige kwa sababu Jeshi la Polisi limejipanga vizuri,” alisema.

Amewaonya wanasiasa wanaohamasisha wananchi walinde kura, akisema watakumbana na nguvu ya jeshi hilo.

"Wanaolinda kura ni mawakala wao. Kila chama kimepeleka mawakala. Kuna baadhi ya vyama vinaona vimeshindwa, vinaanza kuleta uvunjifu. Sisi polisi tunasema atakayeshinda ndiye atakuwa kiongozi," amesema.

Amewataka wadau, ikiwemo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na mawakala kutimiza wajibu wao ili kuepusha vurugu.

"NEC itimize wajibu wake, wasimamizi watimize wajibu, mawakala watimize Wajibu,” amesema.