Sitashangaa Mzee Sumaye akiamua kurejea CCM

Sunday December 1 2019Julius Mtatiro

Julius Mtatiro 

By Julius Mtatiro

Waziri Mkuu mstaafu Fredrick Sumaye anaweza kurejea CCM – huu ni mtizamo wangu unaotokana na uzoefu wangu wa miaka kumi wa kufanya siasa za upinzani nchini Tanzania. Ziko sababu za msingi na dhahiri.

Unaweza kujiuliza kwa nini nimehitimisha kirahisi namna hiyo. Unaweza kujiuliza kwa nini nimeyasema haya leo hii, majibu yake yatakuwa sahihi pale jambo hilo likitokea.

Watu wengi walioko kwenye vyama vya upinzani Tanzania pia wanalitegemea jambo hilo, hasa kwa sababu mshirika wake mkubwa, Edward Lowassa, ambaye pia ni waziri mkuu mstaafu alisharejea CCM.

Urejeaji wa Sumaye si jambo la ajabu, ni rahisi zaidi. Jambo la ajabu na ambalo lingeleta mshangao ni kusikia mtu kama Mtatiro aliamua kujiunga CCM na kuachana na upinzani, jambo la ajabu na lisilotarajiwa kabisa. Kwa hiyo, kama yasiyotarajiwa yalitokea, basi yanayotarajiwa yanasubiriwa.

Ni rahisi zaidi kwa sababu siasa za upinzani ni ngumu. Ngumu sana ndani ya vyama vya upinzani vyenyewe na ngumu hata nje ya vyama vyenyewe, yaani upinzani wa Tanzania una mapambano makubwa sana ya ndani, viongozi kwa viongozi, wanachama kwa viongozi na aina nyingi za mapambano – halafu vyama hivyo vikitoka kwenye mapambano ya ndani vina kazi ya ziada ya kupambana na chama kikubwa – CCM.

Sumaye aliondoka CCM na kujiunga upinzani kutokana na upepo wa kisiasa, kwa sababu mwaka 2015 ulionekana kama mwaka rahisi zaidi wa kuiangusha CCM, jambo hilo likashindikana, kwa hiyo lengo lake kuu na viongozi wengi walioondoka CCM kuelekea upinzani halikufanikiwa. Kwa hiyo Sumaye hana cha kufanya upande wa upinzani.

Advertisement

Yanayojiri sasa

Kinachojiri hivi sasa ndani ya upinzani na hasa Chadema, ni kile nilichokiongelea hapo juu na kile ambacho nimekichukia sana siku zote na mara zote nilipokuwa upinzani; mapambano makubwa ya madaraka, kuhodhi madaraka na kukosa mipango endelevu na ya muda mrefu.

Leo, waziri mkuu mstaafu amegombea nafasi ndogo ya uongozi ndani ya chama, uenyekiti wa kanda ya Pwani, amekataliwa. Mbaya zaidi hakuwa na mpinzani. Walichomfanyia wapiga kura ni kile kinachoitwa demokrasia ya uchaguzi lakini ambacho wengi tunajua ni ‘figisu za uchaguzi’.

Kiuchambuzi, wajumbe wa kikao husika kilichomkataa Sumaye walifanya hivyo si kwa sababu hawamtaki, la hasha! Sababu halisi ambayo mtu yeyote aliyewahi kufanya siasa za upinzani Tanzania atakwambia ni kosa la kugusa maslahi mapana ya chama chake.

Siasa za upinzani za Tanzania ni kuwa na chama ndani ya chama, chama ni hiki cha nje ambacho kila mwanachama anaamini ni sehemu yake lakini chama cha ndani ni kile cha wenyewe.

Mifano zaidi

Ni kama tu vile nikizungumzia siasa za ndani ya CUF, chama nilichokaa kwa miaka 10 nikijifunza uongozi na kujifunza siasa, ambamo kwa hakika upande wa Tanzania Bara kulikuwa na CUF inayoonekana kwa kila mtu lakini ndani yake kukiwa na CUF ya ndani ambayo inaongozwa na Profesa Ibrahim Lipumba.

Na upande wa Zanzibar kumekuwa na CUF ambayo wananchi wote wanaiona hadharani lakini kwa ndani kuna ile ya Maalim Seif.

Siasa za chama ndani ya chama ni moja ya mambo yanayovifanya vyama vya upinzani vya Tanzania vinakuwa dhaifu, na visivyoweza kukabili mapambano ya kisiasa.

Ndani ya Chadema pia, kuna shida hiyohiyo, kuna chama ndani ya chama. Yaani, ile ya wanachama kindakindaki lakini ndani ya kuna chama ndani ya chama. Ili uwe salama kwenye vyama vyetu vya upinzani, unapaswa kuwa mwanachama wa chama cha nje, ukihoji ya ndani ni kosa.

Kosa kubwa ambalo mtu yeyote aliyeko upinzani anaweza kulifanya, ni kujisahau na kugusa maslahi yoyote ya chama ndani ya chama, au chama cha wenye chama. Maslahi hayo mara nyingi yanahusu kuhoji matumizi ya fedha na kugombea nafasi nyeti.

Kinachomkuta Sumaye

Ni kilekile nilichokisema hapo juu, amegusa maslahi ya chama ndani ya chama. Kwa kinywa chake amekiri kuwa amepigiwa kura za hapana na kukataliwa kuwa mwenyekiti wa Pwani kwa sababu pia alichukua fomu ya kugombea uenyekiti wa taifa, jambo ambalo linaangukia kwenye yale masuala machache ambayo ukiyafanya upinzani huwezi kubakia salama.

Kwa upinzani ziko nyadhifa ambazo ni za kudumu kwa watu fulani, hadi pale watakapochoka wenyewe na waweze kupata watu wa kuwaachia nyadhifa hizo, wakikosa watu wa kuwapa huwa ni rahisi kumwaga mboga na ugali na kuvunja chama, kama ilivyovunjika CUF.

Sumaye anafahamu kuwa, hana nafasi tena ndani ya Chadema, haaminiki na ameshafanya kosa ambalo litamgharimu akiwa ndani kwa muda mrefu. Bahati yake ni kuwa, ameshakuwa waziri mkuu wa nchi hii na ana nafasi ya kipekee katika mfumo wa kidola, kiserikali na katika chama kinachoongoza dola, huko ndiyo kwao na hatakuwa na chaguo lingine zaidi ya kurejea na kupumzika.

Sumaye hataziweza riwaya na tamthiliya za siasa za ndani ya upinzani nchini Tanzania, ameshajionea mwenyewe kuwa vyama vya upinzani vinatumia nguvu kubwa mno kupambana ndani ya vyama na kulinda nafasi za watu fulani, kuliko nguvu zinazotumiwa kwenye siasa za jumla za kitaifa.

Haya yanayomkuta Sumaye leo, yameikuta orodha ya makumi na makumi ya viongozi wa upinzani ambao waliwahi kugusa maslahi ya chama ndani ya chama kwa wenye chama.

Julius Mtatiro ni Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma. Simu; +255787536759, Barua pepe; [email protected]

Advertisement