VIDEO: Skendo ya elimu, wanafunzi 18 sekondari hawajui kusoma

Same. Kwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza au cha pili, suala la kusoma na kuandika huwa si tatizo kabisa.

Lakini katika dunia ya sasa hiyo inaweza kuwa nadharia, katika mazingira halisi kuna baadhi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza na pili hawajui kusoma wala kuandika.

Na ndio maana huwa ni jambo la kushangaza na huzuni kwa mzazi anapoambiwa mwanaye wa kidato cha kwanza au cha pili hajui kusoma wala kuandika wakati alifaulu mtihani wa darasa la saba na kuonekana anazo sifa stahiki.

Katika shule ya Sekondari Lugulu iliyopo wilayani Same, Kilimanjaro wamegundulika wanafunzi 18 wa kidato cha kwanza na pili ambao hawajui kusoma na kuandika.

Mwananchi lilipopata taarifa hizo, lilimtafuta mkuu wa shule hiyo, Nduga Makenji ambaye alikiri kuwepo kwa tatizo hilo.

Mwalimu huyo alisema kwa upande mwingine tatizo hilo linachangia shule hiyo kufanya vibaya katika mitihani yake ya hatua mbalimbali.

Mwalimu Makenji alisema shule hiyo karibu kila mwaka hupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza ambao hawajui kusoma wala kuandika.

Alisema kutokana na tatizo hilo, ofisi yake huamua kuwasaidia kwa kuanza kuwafundisha kusoma na kuandika wenye changamoto hiyo ili kuwajengea upya msingi wa elimu.

Alifafanua kuwa wanakumbana na tatizo kubwa la utoro wa wanafunzi wengi na baadhi yao huzua ugomvi na walimu pale wanaposhindwa kufanya kazi wanazopewa darasani.

“Hapa shuleni kuna wanafunzi zaidi ya 18 wa kidato cha kwanza na pili hawajui kusoma wala kuandika, sasa wanafunzi wa namna hii wanaposisitizwa kusoma zaidi wanakuwa watoro wa mara kwa mara darasani, unaweza kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi darasani, lakini wengi wao hawafiki shule na kuhudhuria vipindi kutokana na kutojua kusoma na kuandika,” alisema Mwalimu Makenji.

“Na hii inapelekea wanafunzi hao sasa kutokuwa na nidhamu na mara nyingi wamekuwa wakileta ugomvi na walimu wao kutokana na kusisitizwa mara nyingi kusoma na kuandika, matokeo yake wanaingia kwenye ugomvi na walimu pale wanapopewa kazi za kufanya na kushindwa kutekeleza.

“Sehemu ambayo Serikali inapaswa kuweka juhudi kubwa zaidi ni shule za msingi ili kuhakikisha mwanafunzi anajua kusoma, kuandika na kuhesabu kwani akifika sekondari inakuwa rahisi kwake kuelewa mambo kirahisi maana sisi huku tunajua tayari ameshavuka KKK (kusoma, kuandika na kuhesabu),” alisema Mwalimu Makenji.

“Tunaomba Serikali ibadili utaratibu wa mitihani, hata kama maswali ya kuchagua yapo yasiwe mengi sana yakamsababisha mwanafunzi hali ya (kubahatisha) ku-guess ikawa ni kubwa na kufaulu hata kama hajui, waweke maswali ya kujieleza mengi ili kutathmini uelewa wake,” alisema.

Baadhi ya wanafunzi hao waliozungumza na Mwananchi walisema changamoto kubwa iliyosababisha wao kutojua kusoma na kuandika inatokana na kukosa walimu wa kuwafundisha.

“Mara nyingi unakuta mwalimu akiingia darasani anafundisha somo moja tu, halafu hayo mengine hatufundishwi kutokana na kwamba walimu ni wachache, masomo mengine hatufundishwi kabisa,” alisema mmoja wa wanafunzi hao ambaye tunahifadhi jina lake.

Mratibu Elimu Kata, Eliesa Semshitu alisema tatizo hilo limekuwa likijitokeza mara nyingi, lakini wanafanya jitihada kutatua changamoto hiyo. Alisema changamoto kubwa iliyopo shule za msingi ni kuwa na walimu wachache na kwamba uwiano wa wanafunzi hauendani na idadi ya walimu .

Alisema sababu kubwa ya wanafunzi wengi kufaulu darasa la saba huku wakiwa hawajui kusoma na kuandika inatokana na uwepo wa maswali mengi ya kuchagua kwenye mitihani yao ya Taifa.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, ofisa elimu wilaya ya Same, Happiness Laizer alisema hana taarifa hizo na akakata simu.

Mkurugenzi wa halmashari hiyo, Annaclaire Shija alisema “nipeni muda nifuatilie kwa undani jambo hili.”

Mwaka 2018, matokeo ya kidato cha nne kwa shule hiyo ya sekondari kitaifa hayakuwa mazuri, ilishika nafasi ya 3,476 kati ya shule 3,488 zilizofanya mtihani.

Halikadhalika kimkoa, ilishika nafasi ya 269 kati ya shule 270 zilizopo mkoani Kilimanjaro huku kiwilaya ilijikuta ikishika nafasi ya 49 kati ya shule 50.