Soko la Kariakoo, bandari ya Dar zanyooshewa kidole

Kaimu Mwenyekiti wa TPSF, Angelina Ngalula

Muktasari:

Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) na Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (Taffa) kimewasilisha serikalini hali ilivyo katika soko la Kariakoo na bandari ya Dar es Salaam wakitaka kutizamwe ili kurejesha imani kwa watumiaji wa maeneo hayo.

Dar es Salaam. Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imeitaka Serikali kuunda kamati ndogo kwa ajili ya kuangalia mwenendo wa biashara katika soko la Kariakoo, Dar es Salaam ili kulinusuru kuporomoka kibiashara.

Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Desemba 6, 2019 jijini Dar es Salaam na Kaimu Mwenyekiti wa TPSF, Angelina Ngalula wakati wa mkutano wa mashauriano kati ya serikali, wawekezaji na wafanyabiashara.

Ngalula amesema Kariakoo ni soko la kimataifa lakini hali iliyopo sokoni hapo inasikitisha.

Amesema biashara imeporomoka kwa sababu hakuna mifumo ya kimataifa ya biashara kwenye soko hilo.

"Tunaomba tutengeneze kamati ndogo ya kushughulikia suala la Kariakoo. Unakuta mfanyabiashara ametoka Rwanda kuja kuchukua gari lake bandarini, akichukua gari anapita Kariakoo kununua vitu mbalimbali na kupakia kwenye gari. Watu hao wamekuwa wakisumbuliwa njiani, sasa hawaendi tena Kariakoo," amesema Ngalula.

Ngalula amebainisha kero nyingine ni pamoja na utitiri wa tozo.

Amesema wafanyabiashara wamekuwa wakitoa maoni yao na kuonya kwamba tozo hizo zitaua biashara lakini maoni hayo hayafanyiwi kazi na Serikali ya Tanzania.

Changamoto nyingine amesema wafanyabiashara wamekuwa wakipeleka malalamiko yao kwa mamlaka mbalimbali za Serikali ya Tanzania kuhusu mambo yanayowakwamisha lakini majibu yamekuwa hayatolewi na mamlaka hizo.

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (Taffa), John Urio amewasilisha mapendekezo matatu kwa Serikali, moja likiwa ni kuifanyia marekebisho sheria ya kuanzishwa kwa Shirika la Wakala wa Meli Tanzania  (Tasac).

Urio amesema sekta binafsi haikushirikishwa katika uanzishwaji wa sheria hiyo, matokeo yake biashara katika bandari ya Dar es Salaam imedorora.

"Ombi letu ni kwamba turudie mchakato wa kuorodhesha bidhaa ambazo zitasimamiwa na Tasac kwa mujibu wa sheria hiyo. Kampuni za mafuta zinalipa pesa Tasac kupakua mafuta wakati nao tayari walikuwa na makubaliano na kampuni zingine zenye utaalamu katika eneo hilo," amesema Rais huyo.

Urio amesema kuna msongamano mkubwa wa meli na mizigo katika bandari ya Dar es Salaam kwa sababu hawataki kushirikiana na sekta binafsi katika kutoa huduma.

"Hakuna bandari inayojivunia mizigo kujaa, bandari inatakiwa kuwa empty (tupu), mizigo ikija inatolewa, hiyo inaonyesha efficiency (ufanisi) wa bandari," amesema Urio.

Katika mkutano huo, mawaziri tisa wanasikiliza kisha baadaye watapata fursa ya kuwajibu wafanyabiashara na wawekezaji hao.

Mawaziri wanaoshiriki mkutano ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angella Kairuki; Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

Wengine ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni;  Naibu Waziri wa Madini, Stanislaus Nyongo; Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu; Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega;  Naibu Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Antony Mavunde na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Stella Manyanya.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi