Soma maelezo ya ushahidi wa Freeman Mbowe kuhusu chanzo cha vurugu uchaguzi Kinondoni

Dar es Saalam. Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa uchaguzi mdogo wa marudio wa ubunge jimbo la Kinondoni, ulighubikwa na vurugu na uvunjifu wa sheria zilizosababishwa na makundi matatu wakiwamo Polisi.

Mbowe ambaye ni mwenyekiti wa Chadema aliieleza mahakama hiyo jana akijitetea dhidi ya mashtaka yanayomkabili, likiwamo la uchochezi.

“Uchaguzi ulighubikwa na ukiukwaji sheria, hali iliyosababisha mgombea wetu Salum Mwalimu kushindwa hivyo kufungua kesi Mahakama Kuu,” alidai Mbowe.

Mbowe na viongozi wengine wanane wa chama hicho, wakiwamo wabunge sita wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 112/2018 yenye mashtaka 13.

Akiongozwa kutoa utetezi na wakili wake, Peter Kibatala, Mbowe alidai uchaguzi huo uliofanyika Februari 17, 2018 ulighubikwa na vurugu zilizosababishwa na makundi matatu; Polisi, wasimamizi wa uchaguzi na wasaidizi wake.

Akitoa utetezi wake dhidi ya mashtaka yanayomkabili mbele ya hakimu Thomas Simba, alidai wasimamizi wa uchaguzi waliwanyima mawakala wa Chadema barua za utambulisho, hali iliyosababisha taharuki na sintofahamu.

“Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ambayo vilishiriki kutumia nguvu kukamata mawakala wa Chadema na hata kumkamata mgombea wetu Salim Mwalimu pale Magomeni,” alidai Mbowe.

Alidai mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi uliofanyika Februari 16, 2018 ulifunguliwa na viongozi wa dini ya Kiislam na Kikristo.

Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu ushiriki wa maandamano ya viongozi wa chama chake kutoka viwanja vya Buibui hadi kwa mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni, alidai hakuwapo kwenye maandamano ya wafuasi wa chama hicho.

Mbowe alieleza kuwa kama alitajwa katika mashtaka hayo ya kukataa kutawanyika basi ilikuwa ni kwa hisia kwa sababu hakuwapo eneo la tukio.

Alidai baada ya kumaliza mkutano wa kufunga kampeni aliindoka uwanjani akiongozwa na polisi kuelekea Makao Makuu ya Chadema, Kinondoni.

Mbowe alidai siku hiyo watu waliohudhuria wakiwa njiani walikutana na wenzao CCM makutano ya barabara ya Morocco na Mwananyamala wakiwa na mgombea wao katika gari la wazi.

Mbowe alidai kuwa wanachama hao wa Chadema walikuwa wakiongozwa na Polisi kuelekea barabara ya Morocco, yeye hakujua kilichoendelea nyuma kwani aliekelea na safari yake ya Makao Makuu ya Chadema, mtaa wa Ufipa, Kinondoni.

Alipoulizwa alifikaje mahakamani hapo, alidai kufikishwa kwake hapo alipigiwa simu ya wito akitakiwa kuripiti Kituo cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

“Kabla ya kupokea wito wa polisi, nilikuwa katika utaratibu wa kufuatilia mawakala wetu kutoka makao makuu ya chama Kinondoni hadi Ngome iliyopo Magomeni,” alidai.

Kuhusu kifo cha Akwilina

Mbowe alidai alipata taarifa kuhusu kifo cha Akwilina Akwiline aliyepigwa risasi katika maandamano hayo kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari na kwamba, taarifa iliyotolewa na kamanda wa polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ilieleza kuwa Polisi inawashilikia askari kuhusu tukio hilo.

“Kwa ufahamu wangu hadi leo natoa ushahidi wangu mahakamani hapa, naweza kusema aliyempiga risasi Akwilina Akwilini ni Polisi hiyo ni kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa kamanda Mambosasa alipofanya mkutano na waandishi wa habari, alisema Jeshi lake linawashikilia baadhi ya askari kwa ajili ya uchunguzi,” alidai Mbowe.

Alidai hajawahi kula njama na washtakiwa wenzake bali waliitwa Polisi kwa nyakati tofauti.

Mbowe alidai hakuna mtu kati ya washtakiwa waliopo mahakamani (huku akiwaonyesha kwa kidole), ambao walikamatwa Mkwajuni.

Bulaya augua

Katika hatua nyingine, upande wa utetezi umeshindwa kumalizia utetezi wa Mbowe kutokana na mshtakiwa Ester Bulaya kuugua.

Wakili Kibatala alieleza kuwa mshtakiwa huyo aliiomba mahakama hiyo iahirishe kesi kutokana na kuugua.

Kutokana na maombi hayo, mahakama itoa dakika 10 ili mawakili wa pande zote kujadiliana kuhusiana na ombi hilo.

Hata hivyo, kutokana na maombi hayo, hakimu Simba alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hadi Novemba 8.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine ni katibu mkuu wake, Dk Vincent Mashinji, naibu katibu mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu na wabunge John Mnyika (Kibamba), John Heche (Tarime vijijini), Halima Mdee (Kawe) na Esther Bulaya (Bunda mjini), Peter Msigwa (Iringa mjini), na Esther Matiko (Tarime mjini)