Somo la hisabati lawatesa watahiniwa darasa la saba 2019

Muktasari:

Somo la Kiswahili laendelea kung’ara wakati masomo ya Hisabati likiendelea kuwasumbua wahitimu wa darasa la saba mwaka 2019.

Dar es Salaam.  Wakati ufaulu katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba mwaka 2019 ukielezwa kupanda, ufaulu katika somo la Hisabati umeshuka kwa asilimia 1.05 ikilinganishwa na mwaka 2018.

Katika somo hilo matokeo yameonyesha kati ya wanafunzi 932, 136 waliopata daraja A hadi C ni asilimia 640.97, wakati waliopata daraja D ni asilimia 25.54 huku asilimia 9.50 wakipata daraja E.

Kama ilivyokuwa mwaka 2018 mwaka 2019 pia watahiniwa wameonekana kufaulu zaidi kwenye somo la Kiswahili ambapo ufaulu ni asilimia 87.25.

Ufaulu huo umebainishwa leo Jumanne Oktoba 15, 2019 na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Dk Charles Msonde alipokuwa akitangaza matokeo ya darasa la saba kwa mwaka 2019.

Somo la Kiingereza limeendelea kuwatesa wanafunzi ambapo licha ya ufaulu kupanda kwa asilimia chache ikilinganishwa na mwaka jana bado somo hilo  limekuwa la mwisho.

Mwaka 2019 ufaulu katika somo hilo ni asilimia 53.21 ikilinganishwa na mwaka 2018 ambapo ufaulu ulikuwa asilimia 49.63.