Spika Ndugai arudisha kamati zote Dodoma

Muktasari:

Spika Ndugai awaita Kamati za Bunge kurudi Dodoma huku akisisitiza wakiwa jijini hapo waache kujichanganya kwenye makundi ya mitaani kama hotelini na maeneo mengine

Dodoma. Spika wa Bunge, Job Ndugai ameziita Kamati za Bunge zilizoko kwenye ziara mikoani, zirudi Dodoma na kazi nyingine zitafanywa kwa njia ya mtandao.
Katika taarifa yake kwa waandishi wa habari leo Machi 19, 2020, Ndugai amesema hali hiyo inatokana na tishio la ugonjwa wa corona ambao umeshaingia nchini.
Spika Ndugai amesema utaratibu wa namna ya kuendesha mkutano wa Bunge utaelezwa baadaye lakini akasisitiza Machi 31, 2020 mkutano utaanza kama ratiba inavyoonyesha huku ukitaraji kuwa na mabadiliko katika uendeshaji wake.
Amesema uchambuzi wa bajeti ya serikali hautaathiriwa kwa namna yoyote kwani wamejipanga na baadhi ya maeneo watafanya kwa njia ya mtandao inapobidi.
“Huu ndiyo wakati wa wananchi kuona haja ya kuleta bungeni watu ambao wamesoma kwa kweli angalau wawe na uwezo wa kutumia mitandao maana sasa mambo yanabadilika kila kukicha,watu wajue kuwa tumeshavuka mto Yordani na sasa tuko ng’ambo ya pili,” alisema Ndugai.
Kuhusu namna ya kuendesha mkutano huo, amesema siku za Bunge zikikaribia atatoa utaratibu mpya kupitia vyombo vya habari lakini akaonya wabunge wakiwa Dodoma waache kujichanganya zaidi kwenye hoteli na maeneo yenye mikusanyiko badala yake wawe na tahadhari kubwa.
Kiongozi huyo amesema mbali na kuweka vitakatisha mikono na vifaa vya kupimia joto, maeneo ya Bunge kumewekwa mahema maalumu yatakayotumika kuwapumzisha wabunge au wageni wengine watakaoonekana kuwa na dalili za ugonjwa huo.