Stamico wafanya biashara ya Sh24 bilioni Desemba 2019

Muktasari:

Waziri wa Madini nchini Tanzania, Dotto Biteko amesema Shirika la Madini la Taifa (Stamico) limeanza kuzalisha faida baada ya Serikali kubadilisha uongozi.


Dodoma. Waziri wa Madini nchini Tanzania, Dotto Biteko amesema Shirika la Madini la Taifa (Stamico) limeanza kuzalisha faida baada ya Serikali kubadilisha uongozi.

Akizungumza bungeni mjini Dodoma leo Jumatano Januari 29, 2020, Biteko amesema awali shirika hilo lilikuwa na tatizo la utendaji, kwamba kuna mambo yaliyosababisha lishindwe kufanya  kazi wa ufanisi.

Amebainisha kuwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 1970 halijawahi kujiendesha kwa faida mpaka utendaji wake ulipobadilishwa.

“Tumeshaanza kufanyia kazi. Shirika kwa muda mrefu lilikuwa halina mwenyekiti wa bodi ila kwa sasa ameshateuliwa na sisi tunaangalia menejimenti nzima,” amesema.

Amesema mpaka linafanyiwa maboresho, lilikuwa na madeni ya Sh34 bilioni lakini Desemba 2019 limefanya biashara ya Sh24 bilioni na ndio sababu ya kuweza kutoa gawio serikalini.