Stempu za kielektroniki zimeongeza makusanyo ya kodi

Bariadi. Matumizi wa stempu za kieletroniki zimeongeza makusanyo ya mapato, kupanua wigo wa kodi na kudhibiti mianya ya udanganyifu.

Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Agosti 8, 2019 katika Viwanja vya maonyesho ya Nane Nane yanayofanyika Kitaifa katika viwanja vya Nyakabindi Wilayani Simiyu, Ofisa Elimu na Huduma kwa walipa kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Godfrey Kumwembe amesema mfumo huo ulioanza kutumika kwa bidhaa za sigara, bia, mvinyo, pombe kali na aina zote za vileo, umewezesha mamlaka hiyo kufahamu kiwango halisi cha bidhaa zinazozalishwa na kodi inayostahili kulipwa.

“Mashine maalumu ya TRA yenye stempu hufungwa kwenye mitambo ya uzalishaji na kybandika stempu kwenye kila bidhaa inazozalishwa nchini. Hii hutuwezesha kujua kiwango halisi cha uzalishaji na kiwango cha kodi," amesema Kumwembe.

TRA imeanza kutumia mfumo huo baada ya Serikali kutunga kanuni ya stempu za kielektroniki mwaka 2018.

Mwaka wa fedha wa 2018/19, TRA  ilikusanya Sh15.9 trilioni kati ya lengo la kukusanya Sh18 bilioni kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Elimu na Huduma kwa mlipa kodi, Richard Kayombo.

Kutokana na kuonyesha mafanikio katika vileo, Kumwembe amesema  stempu za kielektroniki zinazoweza kuhakikiwa na mteja kupitia AAP maalumu ya Hakiki Stempu itaanza kutumika kwenye vinywaji baridi ikiwemo soda, maji, juisi pamoja na CD/DVD.

Kamishna wa Uchambuzi wa Sera kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Mgonya Benedicto alisema mfumo wa kuhakiki stampu kielektroniki kupitia simu za kiganjani, utawadhibiti wazalishaji na wafanyabiashara wasio waaminifu waliokuwa wakibandika stempu bandia kwenye bidhaa zao na hivyo kuikosesha Serikali mapato.

“Kila mwenye simu janja ataweza kuhakiki iwapo stempu iliyobandikwa kwenye bidhaa ni halali na imetoka TRA. Hii itasaidia kudhibiti stempu bandia na hivyo kuongeza mapato ya Serikali kupitia kodi na ushuru mbalimbali,” amesema Benedicto