Stempu zapaisha kodi ya bidhaa

Tuesday December 3 2019

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Makusanyo ya Serikali ya ushuru wa bidhaa na kodi ya ongezeko la thamani (Vat) katika bidhaa mbalimbali yameongezeka tangu kuanzishwa kwa stempu za kielektroniki (ETS).

Kamishna Mkuu msaidizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Msafiri Mbibo alisema hivi karibuni kuwa mamlaka hiyo ilikusanya Sh77.8 bilioni kwa pombe kali na mvinyo kati ya Februari na Oktoba.

Kiwango hicho kinawakilisha asilimia 33.7 ya ongezeko ikilinganishwa na Sh58.2 bilioni zilizopatikana mwaka mmoja uliopita. Katika kipindi hicho, Vat katika bidhaa hizo zilikuwa kwa asilimia 30.6 yaani Sh23.5 bilioni.

“Huu ni mwanzo tu. Tuna tumaini kadiri muda unavyokwenda, mfumo wa ETS utaongeza wigo zaidi,” alisema Mbibo.

 Serikali ilitangaza mpango wa kuanzisha ETS tangu Juni mwaka jana, Kampuni ya Uswisi (Société Industrielle et Commerciale de Produits Alimentaires (SICPA) ilishinda zabuni ya kuendesha mfumo huo.

Kampuni hiyo ilisaini mkataba na TRA kutoa huduma kwa kuweka mitambo na kusaidia mifumo ya kusimamia ETS. 

Advertisement

Mbibo aliliambia Mwananchi  kuwa TRA inafanya jitihada za kuhakikisha kuwa bidhaa zote zinauzwa kwa kupitia mfumo huo. Mkakati huo unalenga kuondoa kufurika kwa bidhaa sokoni zisizo na ubora.

“Tunajipanga kuweka uwanja sawa kwa wazalishaji wote. Timu yetu inajipanga kuhakikisha tunatekeleza tunayosema,” alisema Mbibo.

Advertisement