Stori ya Harmonize Vs WCB inafanana na mume mdai mahari

MZEE mzima kapenda, akaamua iwe halali, akaoa. Watoto wakazaliwa. Miaka kadhaa baada ya ndoa, mama kaona mume hamuwezi, anaamua kudai talaka.

Ashakum si matusi, mzee mzima akamwambia mkewe:

“Ukitaka kuachana na mimi, kwanza nirudishie mahari yangu na gharama zangu zote za ndoa, jumla Sh500 milioni.”

Mama kwa sababu mume ameshamwona janga na kwa vile anaona pesa ni za kutafuta, anaamua kuuza nyumba zake za urithi alizoachiwa na bibi yake mzaa mjomba, anazichanga na kumlipa.

Ashakum si matusi, mume anatoa sharti lingine: “Umelipa Sh500 ya kuvunja ndoa, ila watoto si wako. Ukitaka watoto waendelee kukuita mama, nilipe mbegu zangu (ashakum) na gharama za kuwalea, vinginevyo kaa mbali nao.”

Makubaliano ya kimkataba kati ya Harmonize na WCB, unaweza kuyafananisha na huyo mume na mamsapu na wake. Madai ya mahari mpaka gharama za ndoa. Kisha mbegu iliyopandwa na kuleta watoto pamoja na ada za kuwasomesha.

Kwa mujibu wa Harmonize, masharti ya kuvunja mkataba yapo katika makundi mawili. La kwanza, ni kuilipa menejimenti ya WCB Sh500 milioni. Pili, kuondoka kama yeye, asitumie jina la Harmonize pamoja na nyimbo ambazo msanii huyo alizirekodi akiwa WCB.

Sharti hilo la pili likawa na vinginevyo, akitaka aendelee kutumia jina la Harmonize na kutumia nyimbo zilizofanywa ndani ya WCB, basi alipe gharama za utengenezaji wa nyimbo.

TUGAWE MAFUNGU!

Fungu la kwanza ni malipo ya Sh500 milioni, bila shaka WCB walitaka kurejeshewa fidia ya kumtengeneza Harmonize kuwa katika ukubwa alionao. Sawa na dai la mahari na gharama za ndoa ambazo jamaa alimdai mkewe aliyeomba talaka.

Fungu la pili ni Harmonize asitumie jina hilo (labda angejiita Konde Boy), halafu asiguse nyimbo zilizorekodiwa WBC, vinginevyo alipe fedha za matengenezo ya nyimbo. Hili limekaa kama la yule mume aliyemdai mbegu mkewe ili watoto wawe wake. Tuanze na fungu la kwanza; Sh500 milioni. Sina ubishi nayo.

Harmonize ni mwanamuziki pia ni ‘brand’;. WCB kama kampuni ya muziki ilimtendea mambo makuu mawili Harmonize.

Kwanza ni WCB kama recording label, ilimfanya Harmonize kuwa mwanamuziki aliye sasa, pili, WCB kama wasimamizi wa masoko ya muziki (imprint), walimjenga Harmonize kuwa brand ya kibiashara.

Hivyo, WCB kuhakikisha kunakuwa na kipengele cha kutaka fidia ya uwekezaji wao kama Harmonize au msanii mwingine wanayemsimamia, anapotaka kuondoka si la kubishaniwa. Kwa digrii nyingi, WCB wana haki.

Walimchukua Harmonize ambaye hakuna aliyekuwa anamjua. Sasa hivi anaondoka kila mtu anamjua. Ni brand inayotengeneza pesa kila siku. Wangekuwa mazezeta kama wangeruhusu kipengele cha msanii kuondoka anapoamua bila kubanwa na deni lolote la kulipa.

Ambacho kinaweza kubishaniwa ni kiasi, je ni kikubwa au kidogo? Hilo jibu wanalo Harmonize na WCB. Hata hivyo, ndivyo walikubaliana na wakasaini mkataba.

Tuje fungu la pili; kulipia gharama za matengenezo ya nyimbo ili awe huru kutumia jina la Harmonize na nyimbo zote ambazo alizirekodi akiwa WCB. Hili ni sawa na mume kudai malipo ya mbegu zake na malezi ili mke awe na uhuru wa kuendelea kuwa mama wa watoto wake.

Hatubishani WCB waliwekeza fedha kutengeneza nyimbo za Harmonize. Hata hivyo, nyimbo ni uwekezaji wa fedha na sanaa.

Nani mwekezani wa fedha? Jibu ni WCB. Aliyewekeza sanaa ni Harmonize. Hapa hatumtaji mtayarishaji ambaye naye sanaa yake imetumika kuupika wimbo usikike kama ulivyo. Sanaa ya prodyuza (mzalisha muziki), imo ndani ya fedha za WCB.

Tunaweza pia kukubaliana WCB wamewekeza sanaa katika nyimbo za Harmonize. Iwe kwa studio, kumlipa prodyuza au hata kuzijenga nyimbo pamoja. Kwamba Harmonize hajaandika na kutunga nyimbo peke yake bila ushirika wa timu ya WCB.

Ni kama ambavyo mama hapati mtoto peke yake bila ushirikiano wa baba. Vivyo hivyo, baba si mwenye mtoto bila mama. Mtoto ni uwekezaji wa baba na mama.

Inapotokea baba anataka awe mmiliki wa watoto peke yake na eti, kama mama anataka awe mmiliki wa watoto lazima alipie mbegu za baba na gharama za kumlea. Kisha baba anataja fedha za mbegu zake pamoja na uwekezaji wa malezi.

Hayo madai ya baba ni utani ambao haujazaliwa. Haukuwepo milenia zote mbili zilizopita na hautarajiwi kuzaliwa Karne ya hii ya 21. Labda milenia ya nne, kama itakuwa na kizazi kilichokata ringi zaidi.

Baba anapodai alipwe mbegu zake, ina maana hao watoto wanakuwa sio wa kwake? Ni kama WCB kudai walipwe gharama za uwekezaji wa nyimbo, ina maana hawajanufaika chochote kupitia nyimbo?

Wimbo unapotoka na kutengeneza fedha, kila upande unanufaika kulingana na uwiano uliokubaliwa kimrabaha. Kila wimbo ulipotoka, WCB walipata na Harmonize aliingiza. Kama ambavyo mtoto akizaliwa, baba anamwita baba, mama ni mama. Kila mmoja anastahili yake.

Nyimbo zimefanya biashara, mmepiga hela wote. Miaka kadhaa baadaye, unamwambia msanii alipe fedha za kutengeneza nyimbo ili awe huru kuzitumia aendako. Kama baba kudai mbegu zake ili mama awe huru kwa watoto wake, ilihali wote waliwekeza kupata watoto na wote ni wanufaika kutokana na watoto.

ISIVYO SAWA!

Madai ya pili ndio yanafanya kuhoji madai ya kwanza yanahusu nini? Kama Harmonize analipia Sh500 milioni awe huru kuondoka WCB, kivipi tena alipie gharama za nyimbo ndipo awe na uhuru na nyimbo zake pamoja na jina lake?

Tunakubaliana, Harmonize amejengwa na WCB, hivyo walitaka fidia kwa kuvunja mkataba. Sh500 milioni imetajwa. Kisha, WCB wanataka malipo ya uwekezaji wa kila nyimbo. Sasa Sh500 milioni za nini?

Harmonize amesema hakutaka ubishani, ndio maana aliamua kuuza nyumba zake tatu kulipa madai aliyotajiwa. Pongezi kwake. Hata hivyo, angekuwa mwingine angehoji, WCB wanarudisha nini?

Kama WCB na Harmonize waliwekeza fedha na sanaa kutengeneza nyimbo, kisha kila mmoja akanufaika kutokana na mrabaha. Ikiwa sasa Harmonize amelazimika kuzilipia nyimbo hizo ili ziwe mali yake, maana yake Harmonize ni mwekezaji pekee wa nyimbo zake.

Kwamba WCB wao walimkopesha tu Harmonize uwekezaji wa nyimbo na amelipa. Kama ndivyo, je, WCB watarejesha fedha za mrabaha ambazo miaka yote wamekuwa wakipokea kutokana na nyimbo za Harmonize?

Kwa kifupi WCB hawajamtendea Harmonize kitu kizuri. Walimsainisha mkataba wa hovyo nyakati ambazo alikuwa hana ufahamu wa kutosha. Ndio maana baada ya kupanuka mawazo, amegundua ananyonywa.

Ni darasa kwa wasanii wachanga kutokimbilia kusaini mikataba bila ufahamu wa kutosha. Miaka ya baadaye unagundua unanyonywa halafu ukitaka kuuvunja, unanyonywa zaidi ili uwe huru.