Sudan Kusini yakwamisha vigogo EAC kukutana Tanzania

Saturday February 22 2020

 

By Filbert Rweyemamu, Mwananchi [email protected]

Arusha. Mkutano wa kawaida wa 21 wa marais wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliokua umepangwa kufanyika Jumamosi Februari 29, 2020 umeahirishwa hadi utakapopangwa tena ili kupisha Serikali ya Sudan Kusini kuunda Serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Sekretarieti ya EAC leo Jumamosi Februari 22, 2020 na kusainiwa na Ofisa Habari Mwandamizi, Simon Owaka imesema kuahirishwa kwa mkutano huo ambao ulikua ufanyike makao makuu wa jumuiya hiyo jijini Arusha, Tanzania ni kuitikia maombi ya nchi ya Sudan Kusini.

“Kuharishwa kwa mkutano wa 21 wa wakuu wa nchi za EAC ni maombi ya Jamhuri ya Sudan Kusini ambao wameomba wapate muda wa kuunda serikali ya mpito ya pamoja kati ya serikali na makundi ya wapinzani,” amesema Owaka

Kwa mujibu wa Mkataba wa EAC Ibara ya 11 inataka uamuzi unaofikiwa kuwa wa maridhiano na nchi zote sita wanachama zishiriki katika mikutano ya ngazi zote, kutokuwapo kwa nchi moja katika mkutano huo kunamaanisha akidi kutokutimia.

Nchi hiyo imekua katika mgogoro wa madaraka kati ya Rais Salva Kiir na aliyekua Makamu wake, Riek Machar miaka miwili baada ya kuwa taifa huru kutoka nchi ya Sudan (Khartoum) mwaka 2011 na kusababisha mamia ya watu kupoteza maisha na wengine kuhama makazi yao.

Sudan Kusini ilijiunga rasmi na EAC mwaka 2016 katika hafla iliyofanyika Ikulu ya jijini Dar es Salaam wakati huo Rais John Magufuli akiwa mwenyekiti wa wakuu wa nchi wanachama wa EAC.

Advertisement

 

Advertisement