Sugu amjibu Dk Bashiru madiwani 11 Chadema kuhamia CCM

Muktasari:

Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu Sugu amemtumia salamu katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally akibainisha kuwa madiwani 11 wa Chadema katika Jiji la Mbeya kuhamia chama tawala hakuwezi kubadili mapenzi ya wananchi wa Mbeya kwa Chadema.


Dar es Salaam. Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu Sugu amemtumia salamu katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally akibainisha kuwa madiwani 11 wa Chadema katika Jiji la Mbeya kuhamia chama tawala hakuwezi kubadili mapenzi ya wananchi wa Mbeya kwa Chadema.

Sugu ametoa kauli hiyo leo Jumanne Februari 25, 2020 alipozungumza na Mwananchi ikiwa ni siku moja baada ya madiwani hao, akiwemo Meya wa Jiji la Mbeya, Mchungaji David Mwashilindi kujivua nyadhifa zao na kuhamia CCM.

Madiwani hao walipokelewa jana Jumatatu na Dk Bashiru katika ofisi za makao makuu ya CCM jijini Dodoma huku mtendaji mkuu huyo wa CCM akisema hizo ni salamu kwa Sugu kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba, 2020.

Madiwani hao  na kata zao kwenye mabano ni Mwashilindi (Nzovwa), naibu Meya, Fanuel Kyanula (Sinde); Fabian Sanga (Ghana); Anyandwile Mwalwiba (Isanga);  Dickson Makilasa (Ilomba); Constantine Mwakyoma (Kalobe); Furaha Mwandalima (Ilomi); Anderson Ngao (Mwasanga); Ibrahim Mwampwani (Isyesye); Henry Mwangambaku (Forest) na Kigenda Kasebwa (Viti Maalumu).

“Dk Bashiru mwenyewe Mbeya haijui, ameuziwa mbuzi kwenye gunia, amechukua watu ambao hawana ‘future’ kwenye maeneo yao na wala wasingepita kwenye kura za maoni.”

“Unachoweza kujiuliza kwa nini Bashiru  haongezi wapiga kura lakini  anahangaika kutafuta wanaopigiwa kura?” amehoji Sugu.

Sugu amesema madiwani hao kuondoka Chadema kumezidisha hasira kwa wakazi wa Mbeya, “ambao sasa wameongezeka kujiandikisha, yaani mimi sasa hivi malengo ni kufikia Juni niwe nimesajili wananchi 100,000. Yeye muache ahangaike na wapigiwa kura badala ya wapiga kura.”

Amesema licha ya madiwani hao kuondoka, bado wana idadi kubwa ya madiwani hivyo wataendelea kuongoza Jiji hilo.

“Suala la ubunge na kura za urais Mbeya tulikwisha kulimaliza tangu mwaka 2010, wakiwa hawaamini basi wasubiri wataona,” amesisitiza.

Amesema Dk Bashiru anatakiwa kujikita zaidi kumshauri mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli ili  atekeleze ahadi alizowaahidi wananchi katika kampeni za mwaka 2015, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara ya  Mapelele kata ya Ileni jimbo la Mbeya Mjini. Amesema barabara hiyo haijajengwa licha ya ahadi kutolewa mwaka 2015.