Sura mpya Chadema zakuna wadau

Tuesday December 3 2019

 

By Waandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Moshi/Dar. Uchaguzi wa viongozi wa kanda za Chadema umemalizika kwa sura mpya kadhaa kuibuka na ushindi, hali ambayo imeelezwa kuwa itakuwa chachu ya chama hicho kufikia malengo yake ya kisiasa.

Chadema ilihitimisha uchaguzi huo juzi kwa kanda zake tisa kati ya kumi kupata viongozi baada ya waziri mkuu wa zamani, Frederick Sumaye kuanguka katika uchaguzi wa Kanda ya Pwani aliosimama peke yake.

Pwani walishindwa kumpata mwenyekiti baada ya aliyekuwa mgombea pekee kwenye nafasi hiyo kupigiwa kura za hapana 48 na ndio 28.

Kati ya wenyeviti hao tisa, wawili pekee Mchungaji Peter Msigwa (Nyasa) na Ezekia Wenje (Victoria) ndio waliofanikiwa kutetea nafasi zao, huku sura mpya zikimjumuisha Esther Matiko atakayeongoza Kanda ya Serengeti baada ya kumbwaga John Heche.

Wenyeviti wengine ni Godbless Lema (Kaskazini), Selemani Mathew (Kusini), Lazaro Nyalandu (Kati), Hafidh Saleh (Pemba) na Said Mzee Said (Unguja).

Kuhitimishwa kwa uchaguzi huo kunatoa fursa ya kuanza harakati za uchaguzi wa viongozi wa mabaraza ya vijana, wazee na wanawake kuanzia Desemba 10 na utahitimishwa Desemba 18 wakati viongozi wa juu watakapochaguliwa.

Advertisement

Wachambuzi wa siasa wanaona sura hizo mpya na za zamani ni chachu ya kukifanya chama hicho kusonga mbele zaidi wakati huu kikielekea katika uchaguzi mkuu mwakani.

“Asilimia kubwa ya wenyeviti hao ni vijana wanaomuunga mkono Freeman Mbowe,” alisema mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Faraja Kristomus.

Alisema hali hiyo itasaidia shughuli za chama hicho kwenda kwa ufanisi, kama suala la wabunge kuchangia chama na hakutakuwa na mapingamizi.

“Ingawa sijajua Pwani atashinda nani, lakini hawa waliochaguliwa wote watiifu kwa Mbowe. Endapo Mbowe akifanikiwa kutetea nafasi yake, hatakuwa na kazi katika utekelezaji wa majukumu yake kwa sababu walioko chini yake wanamtii,” alisema.

“Naona uwezekano mkubwa wa viongozi hawa kuzungumza lugha moja na mwenyekiti wao. Hii ni timu ya watiifu na watafanya mikakati kwa pamoja.”

Hata hivyo, alisema mwaka 2020 Chadema itakabiliwa na changamoto, ikiwa ni pamoja na kujiimarisha kuanzia ngazi ya chini ili wanachama wake waweze kukiamini .

Alisema miaka minne imekuwa migumu kwa wapinzani, hivyo Chadema italazimika kufanya kazi ya ziada kuhakikisha inarudi katika hali ya kawaida hasa katika kipindi hiki ambacho hakina viongozi wa ngazi ya chini baada ya kususia uchaguzi wa serikali za mitaa, vitongoji na vijiji uliofanyika Novemba 24.

“Safu hii mpya ya viongozi imeondoa minong’ono ya kwamba wageni hawapewi nafasi ndani ya Chadema,” alisema.

“Kingine, Chadema watalazimika kutibu majeraha ya 2015 yaliyosababishwa na wageni waliojiunga na chama na kuondoka. Itabidi wawabembeleza wanachama wao waliowanyima nafasi mwaka 2015.”

Mtazamo huo unalingana na wa Matiko aliyesema ushindi wake unachagizwa na uthubutu na ujasiri katika kuamua mambo yenye mustakabali kwa taifa na wakati mwingine humuweka matatani.

“Ujasiri wa kusimamia na hata kama itagharimu maisha yangu nitasimamia,” alisema.

“Nikiamua leo natamani kuwa wakili, nitahakikisha nafikia huko. Kama ni nafasi imetangazwa nitashiriki bila kuogopa,” alisema mbunge huyo wa Tarime Mjini

Matiko alisema ukiwa mwenyekiti wa kanda, unakuwa mjumbe wa Kamati Kuu na unafanya uamuzi.

“Vijana wanapata mwamko, tukiamua kutumia ujuzi, uwezo na uzoefu tunaweza, hasa ikizingatiwa kuwa Kamati Kuu ndiyo chombo kikuu cha kufanya uamuzi kwa mambo mbalimbali,” alisema.

Naye Lema alisema kuchaguliwa kwake katika nafasi hiyo mpya kunatokana na namna viongozi wake pamoja na wanachama wanavyomwamini namna anavyoweza kukabiliana na changamoto mbalimbali za kutafuta demokrasia ya kweli.

“Nimefurahi kupewa wajibu huu lakini si kwa sababu una raha, ila ni kwa sababu ninaweza kukabiliana na changamoto zake na kuhakikisha taifa letu linakuwa mahali bora zaidi,” alisema mbunge huyo wa Arusha Mjini.

“Ninafurahi angalau kupata nafasi hii maana nchi hii watu wanatambua mchango wangu.”

Naye Wenje alisema atahakikisha katika uchaguzi mkuu 2020 wanapata halmashauri nyingi katika manispaa wanapata madiwani wengi, kura nyingi za wabunge na kura nyingi za urais katika kanda hiyo.

Mchungaji Msigwa alisema ataendelea kukiimarisha chama chake na kutengeneza mshikamano na umoja na kwamba makundi ndani ya chama hicho sasa yaishe.

Advertisement