TCRA yasisitiza usajili laini za simu

Muktasari:

Wananchi wanahimizwa kwenda kusajili laini zao za simu kwa njia ya alama za vidole wakitumia namba ya kitambulisho cha Taifa ambayo inapatikana hata bila kuwa na kitambulisho chenyewe.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), James Kilaba amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kusajili laini zao za simu kwa njia ya alama za vidole.

Kilaba ametoa wito huo leo Desemba 13 jijini Dar es Salaam wakati wa semina maalumu na waandishi wa habari iliyofanyika kwa lengo la kuwajengea uelewa katika kutoa taarifa za usajili wa laini za simu.

Amesema kitu muhimu kinachohitajika ni namba ya kitambulisho cha Taifa ambayo inaweza kupatikana kwa njia mbalimbali ikiwemo kutuma ujumbe mfupi wenye taarifa zako kwenda namba 15096.

"Kuna kundi kubwa la watu ambao namba zao za kitambulisho ziko tayari lakini hawajasajili laini zao na pengine hawajui kama ziko tayari. Huhitaji kwenda Nida ili kupata namba yako ya kitambulisho, unaweza ukatumiwa kupitia simu yako na ukasajili laini yako," amesema Kilaba.

Awali akiwasilisha taarifa ya hali ya usajili hadi kufikia Desemba 10, mkurugenzi wa mambo ya kisekta wa TCRA, Dk Emmanuel Mannaseh amesema laini za simu zilizosajiliwa kwa alama za vidole ni 19,681,086 sawa na asilimia 42. Amesema laini hizo zinamilikiwa na watu milioni 7.6.

Dk Mannaseh amesema laini ambazo wamiliki wake wana namba za utambulisho za Nida lakini hazijasajiliwa kwa njia ya alama za vidole ni 5,599,610 ambazo wamiliki wake ni takribani watu milioni tatu.

Amesema kati ya laini 47,063,602 zinazotumika sasa na kumilikiwa na watu milioni 21.1, laini 21,782,906 zinazomilikiwa na takribani watu milioni 10, hazijasajiliwa kwa alama ya vidole.