TCRA yatoa utaratibu wa kuhakiki laini za simu kabla ya Januari 20

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba

Muktasari:

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewaagiza Watanzania waliokamilisha usajili wa laini zao za simu kwa alama za vidole, kuhakiki upya kwa kupiga namna *106# na kuchukua hatua stahiki kabla zoezi la kuzima rasmi simu ambazo hazijasajiliwa Januari 20 mwaka huu.

Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku tatu laini za simu zisizosajiliwa kwa alama za vidole kufungiwa, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewaagiza Watanzania waliokamilisha usajili wa laini zao kuhakiki upya kwa kupiga namna *106#.

Taarifa kwa umma iliyotolewa leo Alhamisi Januari 16, 2020 na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba imeeleza shughuli hiyo inapaswa kufanyika kabla ya kazi hiyo kuzima rasmi simu ambazo hazijasajiliwa Januari 20, 2020.

“Kama mnavyofahamu, mwisho wa kutumika kwa laini za simu ambazo hazijasajiliwa kwa kutumia namba ya kitambulisho cha taifa (Nida) na kuthibitishwa kwa alama za vidole ni Januari,20, 2020, kama umeshasajili hakiki tena usajili wa laini zako kwa kupiga namba *106# na uchukue hatua stahiki sasa,” imeeleza taarifa hiyo.

TCRA imesema ukomo wa Januari 20, 2020 unawahusu wale tu ambao wana laini za simu sasa (ama kwa ajili ya mawasiliano ya simu au vifaa vyao vya mawasiliano mengine) lakini hawajazisajili kwa kutumia namba ya kitambulisho cha taifa (Nida) na kuthibitishwa kwa alama za vidole.

Hata hivyo TCRA imeeleza mambo muhimu matatu ya kufuatwa huku ikibainisha kuwa zoezi hilo ni endelevu.

“Kwa watakaositishiwa huduma za laini zao za simu Januari 20 wanaweza pia kuendelea na utaratibu wa usajili kwa lengo la ama kurudisha laini zao zitakazokuwa zimefungwa au kupata laini mpya,”

“Kwa watumiaji/waombaji wapya wa laini za simu wataendelea kusajiliwa muda wote na usajili huo kwa kutumia kitambulisho cha taifa na kuhakikiwa kwa alama za vidole, huduma ambayo ni endelevu pia.”

“Kwa wanadiplomasia au taasisi zao ambao hawajakamilisha usajili wa laini zao za simu au zinazotumika kwenye vifaa vyao vya mawasiliano waendelee kufuata utaratibu waliowekewa,” imeeleza taarifa hiyo.”