TEA yatoa mwongozo wanaotaka kuchangia sekta ya elimu Tanzania

Friday January 10 2020

By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mamlaka ya Elimu Tanzania (Tea) imewataka wadau wanaoguswa kuchangia katika sekta  ya elimu kufanya hivyo kwa kupitia mfuko wa elimu unaoratibiwa na mamlaka hiyo ili kuiwezesha Serikali kuwa na takwimu sahihi.

Hatua hiyo itawezesha pia utaratibu misaada inayotolewa na kuisambaza katika shule na taasisi za elimu kulingana na uhitaji.

Hayo yameelezwa leo Ijumaa Januari 10, 2020 na Mkurugenzi wa Tea, Bahati Geuzye wakati akipokea tani tano za mabati kutoka kampuni ya Yalin Global Ltd.

Amesema mamlaka hiyo imeundwa kisheria ikiwa na majukumu kadhaa moja wapo ni kuratibu michango ya elimu nchini.

“Taasisi au mtu binafsi mwenye mapenzi mema na maendeleo ya elimu nchini anaweza kuchangia kupitia Tea na hata mifuko ya elimu iliyoko kwenye halmashauri.”

“Hii itatuwezesha kutambua nani ametoa nini na kinapelekwa wapi, hapo tutaweza kuratibu na kuhakikisha tunazifikia shule zote kulingana na mahitaji,” amesema Geuzye.

Advertisement

Amesema kupitia mfuko huo kila mchangiaji wa elimu anatambuliwa kisheria na kupewa hati ya utambuzi wa elimu.

Gauze amebainisha kuwa hati hiyo inaweza kutumiwa na mchangiaji kuomba nafuu  ya kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha mfuko huo.

“Itakuwa vema endapo wadau wengine wataiga mfano wa kampuni ya Yalin Global Ltd, wamesaidia kwenye miundombinu katika sekta ya elimu na kupitia utaratibu huu tunakuwa na uratibu mzuri na tutayapeleka mabati mabati haya kwenye maeneo yenye uhitaji,” amesema

Kwa upande wake msemaji wa kampuni ya Yalin Global Ltd, Remmy Siyame amesema wametoa msaada huo kama sehemu ya utaratibu wao wa kurudisha kwenye jamii.

“Tumeona tuanze mwaka kwa kusaidia sekta ya elimu tumetoa mabati yenye thamani ya Sh18 milioni na tunatarajia kutoa mengine katika kipindi kifupi kijacho maana kuna mzigo mwingine utaingia hivi karibuni,” amesema Siyame

Advertisement