TEF yataka majeruhi ajali ya moto Morogoro washitakiwe

Muktasari:

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limekemea tabia mbaya ya wananchi kuchukulia ajali kama sehemu ya kujipatia mali kwa njia haramu, katika salamu zao za pole kwa ajali ya moto ilitotokana na ajali ya lori la mafuta mkoani Morogoro.

Dar es Salaam. Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limeeleza kushtushwa na taarifa za vifo vya Watanzania zaidi ya 60 walioungua moto wakati wakichota mafuta kutoka katika lori lililopata ajali eneo la Msamvu, Morogoro, jana Agosti 10, 2019 likitaka waliojeruhia kushitakiwa watakapopona majeraha yao.

Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana usiku Jumamosi na Kaimu Mwenyekiti Jukwaa hiloDeodatus Balile ilisema vifo hivyo vimetokana na tabia mbaya iliyojengeka kwa baadhi ya watu kuchukulia ajali kama fursa ya kujipatia mali kwa njia haramu iliyoanza miaka ya hivi karibuni.

“Tumeshuhudia picha za watu waliofariki kwa kuungua moto zikirushwa kwenye mitandao ya kijamii kinyume cha maadili ya taaluma ya uandishi wa habari na upashanaji habari. Tunakemea tabia hii na kuitaka jamii iache mara moja tabia hii ya kinyama isiyo ya utu,” alisema Balile. 

Balile pia alizungumzia watu zaidi ya 70 waliojeruhiwa katika ajali hiyo akisema wakipona wajiepushe na tabia hii ya uporaji. 

“Ikilazimu, wote watakaopona katika ajali hii washitakiwe kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwao na wengine kuwa ikitokea ajali tunapaswa kusaidia majeruhi na kuokoa mali zao badala ya kupora,” alisema.

“Tunaomba viongozi wa dini, wazazi, viongozi wa kisiasa na jamii kwa ujumla itumie ajali hii kufundisha watoto na vijana maadili mema ya kuwa watu wa msaada mtu anapopata ajali kwa kusaidia majeruhi na kuokoa mali za waliopata ajali badala ya kuwapora,” aliongeza.   

Hadi jana usiku, watu 64 walikuwa  wameripotiwa kufariki huku 70 wakijeruhiwa ambapo baadhi ya majeruhi wamelazwa Hospitali ya Morogoro na wengine wakihamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.