TMA yaeleza mwelekeo wa mvua

Mkurugenzi wa TMA, Dk Agness Kijazi

Muktasari:

Mkurugenzi wa TMA, Dk Agness Kijazi amesema mvua zinatarajiwa kunyesha kuanzia Novemba hadi Aprili mwaka 2021 katika mikoa yenye msimu mmoja wa mvua kwa mwaka

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) imetoa mwelekeo wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka zinazotarajiwa  kunyesha wastani hadi juu ya wastani.

Akizungumza leo  Jumatano, Oktoba 21, 2020 Mkurugenzi wa TMA, Dk Agness Kijazi amesema mvua hizo zinatarajiwa kunyesha kuanzia Novemba hadi Aprili mwaka 2021.

Dk Kijazi ameitaja mikoa inayotarajiwa kupata mvua za msimu mmoja kwa mwaka ni Dodoma, Singida, Mbeya, Songwe, Ruvuma, Njombe, Iringa, Lindi na  Mtwara.

Maeneo mengine ni kusini mwa Morogoro, mashariki mwa Tabora na Katavi yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.

Pia maeneo ya mikoa ya Kigoma, Rukwa pamoja na magharibi mwa mikoa ya Tabora na Katavi yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.

"Hali ya unyevunyevu wa udongo kwa ustawi wa mazao na upatikanaji wa maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji vinatarajiwa kuwa vya kuridhisha katika maeneo mengi," amesema DK Kijazi.

Hata hivyo,  mazao yanaweza kuathiriwa na hali ya unyevunyevu wa kupitiliza, mmomonyoko wa udongo, kupotea kwa rutuba na kutuama kwa maji mashambani yanayotarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani.

Dk Kijazi amesema kutajitokeza uharibifu wa miundombinu ya umwagiliaji kutokana na vipindi vifupi vya mvua kubwa vinavyoweza kukitokeza.

Pia, Dk Kijazi amesema mvua za nje ya  msimu zinatarajiwa kunyesha Januari 2021 katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua ikiwemo mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Dar es Salaam na Kaskazini mwa mikoa wa Morogoro.

Mikoa mingine ya Pwani, kisiwa cha Mafia na Unguja na Pemba.