TMA yataja mikoa itakayonyesha mvua kubwa Tanzania

Muktasari:

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabari wa hali ya hewa kwa siku tano mfululizo kuanzia jana Jumanne hadi Februari 1, 2020 na kubainisha mikoa ambayo inatarajiwa kunyesha mvua kubwa.

Dar es Salaam. Tahadhari imetolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ya kunyesha kwa mvua kubwa kwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Kagera, Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga, Mara, Singida, Dodoma, Manyara, Arusha na Kilimanjaro.

Taarifa ya TMA iliyotolewa jana Jumatano Jamanne Januari 28,2020 ilisema athari zinazoweza kujitokeza ni uharibifu wa miundombinu na mali kwa baadhi ya maeneo, baadhi ya makazi kuzungukwa na maji.

“Hatari kwa maisha ya watu kutokana na maji yanayotiririka kwa kasi au maji yenye kina kirefu, ucheleweshwaji wa usafiri, kusimama kwa muda kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi na kijamii,” ilisema TMA

Kesho Alhamisi Januari 30, 2020 TMA imetoa angalizo la mvua kubwa kwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro. Mikoa hiyo inatarajia pia kunyesha kwa mvua kubwa Ijumaa.

Februari 1, 2020 TMA imesema mvua kubwa inatarajia kunyesha kwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Rukwa, Iringa, Mbeya, Njombe, Manyara, Arusha na Kilimanjaro.