TMDA yaanza kuimarisha mifumo ukaguzi wa dawa nchi za Sadc

Wednesday November 6 2019

Washiriki wa Mkutano wa Mawaziri wa sekta ya

Washiriki wa Mkutano wa Mawaziri wa sekta ya Afya na Ukimwi kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi Kusini mwa Afrika (Sadc) wakiwa katika moja ya mijadala inayoendelea, mkutano huo ulioanza juzi Novemba 4 umetanguliwa na mkutano wa siku tatu wa makatibu wakuu na maafisa wa serikali wa nchi 16. 

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) imeanza kuzipatia mifumo ya kiufundi nchi za Sadc ili ziweze kushirikiana katika sekta ya dawa, vifaa, vifaatiba na vitendanishi.

Desemba, 2018 TMDA ilifikia ngazi ya tatu ya Shirika la Afya Duniani (WHO) katika ubora wa mfumo wa udhibiti wa dawa barani Afrika.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Novemba 6, 2019 katika maonyesho ya mkutano  wa mawaziri wa sekta ya afya na Ukimwi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) meneja mawasiliano na elimu kwa umma wa mamlaka hiyo,  Gaudensia Simwanza amesema mfumo wa Tanzania katika udhibiti unatambulika na ni nchi ya tatu duniani iliyofikia hatua hiyo.

“Kitaalamu wanaita WHO maturity level 3 kati ya ngazi nne ambazo zimewekwa duniani, Tanzania tumefikia. Tunatoa msaada wa kiufundi ili nchi nyingine mifumo yao iimarike waweze kufikia ngazi ambayo Tanzania imefika,” amesema Simwanza.

“Dawa zinazotumika kufubaza makali ya Ukimwi,  TMDA tunasimamia ubora wake, usalama na ufanisi ili tunaposema dawa hii imesajiliwa na inatumika tunakuwa na uhakika.”

Advertisement