TMDA yabaini dawa bandia sokoni, ipo ya malaria

Wednesday November 13 2019

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba  (TMDA) imebaini aina saba za dawa bandia sokoni ikiwemo Sulphadoxine Pyrimethamine (SP) inayotibu malaria.

Hadi leo Jumatano Novemba 13, 2019 mamlaka hiyo imekamata dawa bandia za Sh12 milioni katika maeneo mbalimbali.

Hayo yameelezwa leo Jumatano Novemba 13, 2019 na kaimu mkurugenzi wa TMDA, Akida Khea katika mkutano wake na waandishi wa habari akiwasilisha  ripoti ya ukaguzi wa dawa uliofanyika Oktoba 8 hadi 18, 2019 katika wilaya 33 na Mikoa 20.

“Dawa hizo ni pamoja na inayotibu malaria ya SP ‘Sulphadoxine Pyrimethamine’ dawa za kupaka Sonadem Cream 10gm, Gentrisone Cream 10gm, ALPRIM, Homidium Chloride, Cold Cap na TEMEVAC NDV strain 1&2 (chanjo ya kuku kwa ajili ya ugonjwa wa mdondo),” amesema Khea.

Amesema pia wamebaini uwepo wa dawa za Serikali zenye nembo ya GOT zinazouzwa katika maduka ya watu binafsi na wamekata za Sh481,600 na vifaa tiba vya Sh224,300.

Mrakibu wa Jeshi la Polisi kutoka makao makuu ya upelelezi, Alekunda Urio amesema maeneo yote ambayo dawa hizo zilipatikana, waliokamatwa walifikishwa katika vyombo vya usalama na kesi 19 zilifunguliwa katika vituo mbalimbali vya polisi nchini.

Advertisement

Advertisement