VIDEO: TMDA yakamata dawa zisizo na usajili

Muktasari:

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imekamata dawa na vifaa tiba ambavyo havijasajiliwa vyenye thamani ya Sh48 milioni.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imekamata dawa na vifaa tiba ambavyo havijasajiliwa vyenye thamani ya Sh48 milioni.

Vimekamatwa katika ukaguzi maalum wa dawa, vifaa tiba,  vitendanishi, dawa asili na mbadala uliofanyika Oktoba  8 hadi 11, 2019.

Akizungumza leo Jumatano Novemba 13, 2019 wakati akiwasilisha ripoti ya ukaguzi wa dawa uliofanyika katika wilaya 33 na Mikoa 20, kaimu mkurugenzi wa TMDA,  Akida Khea amesema walikamata dawa za Sh31.9 milioni.

Dawa hizo ni Indowin, vidonge vya dawa yenye mchanganyiko wa Artesunate na Amodiaquine, kapsuli za dawa za Coldwin na dawa ya sindano ya Magnesium Sulphate.

Amesema katika operesheni hiyo walikamata vifaa tiba ambavyo havijasajiliwa vya  Sh16.3 milioni.

“Baadhi ya dawa hizo ni Magnetic Quantum analyser (3), Quantum therapy analyzer pamoja na aina mbalimbali ya kondomu kama vile ultimate condoms, classic maximum protection na prudence condoms,” amesema.