TRA ilivyozungumzia ongezeko la makusanyo miaka minne ya Rais Magufuli

Monday November 25 2019

Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka  ya Mapato

Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka  ya Mapato Tanzania (TRA)  Msafiri Mbibo akisikiliza swali kwa Umakini alilokuwa anaulizwa na Mwandishi wa Habari (Hayupo Pichani) kuhusu Mafanikio ya TRA katika Miaka Minne ya Serikali ya Awamu ya Tano , Mkutano ulifanyika leo Jumatatu (Novemba 25, 2019) Jijini Dar es Salaam.  

By Ephrahim Bahemu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Serikali ya awamu ya tano imeongeza makusanyo ya kodi kiasi cha Sh23.4 Trilioni katika kipindi cha miaka minne ikilinganishwa na miaka minne ya mwisho ya Serikali ya awamu iliyopita.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Novemba 25, 2019 Naibu Kamishina wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Msafiri Mbibo amesema kwa kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2015/16 TRA wamekusanya Sh58.3 Trilioni huku miaka minne nyumba kabla ya hapo makusanyo yakiwa ni Sh34.97 trilioni.

"Wastani wa makusanyo kwa mwezi yameongezeka kutoka Sh850 bilioni hadi Sh1.3 trilioni na mwaka huu wastani huo umeongezeka hadi Sh1.4 trilioni. Mafanikio hayo yanatokana na juhudi za Serikali kuongeza ukusanyaji, kubana mianya ya upotevu wa mapato na kubuni vyanzo vipya," amesema Mbibo.

Vilevile Mbibo amesema katika kipindi cha miaka minne chombo hicho cha ukusanyaji wa kodi kimeongeza idadi ya walipa kodi waliosajiliwa kutoka milioni 2.2 hadi milioni 3.01 huku akisema mfumo wa stempu za kielektroniki umeongeza na kuboresha ukusanyaji wa kodi.

"Miongoni mwa changamoto tulizonazo pamoja na mafanikio tuliyoyapata ni ukwepaji wa kodi wa makusudi, biashara za magendo utaratibu wa kuuza na kununua bila kudai na kutoa risiti za EFD," amesema Mbibo.

Advertisement