TRA wakamata bidhaa za mamilioni kutoka Kenya

Thursday February 13 2020

By Florah Temba, Mwananchi [email protected]

Moshi. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kilimanjaro imekamata bidhaa mbalimbali zilizoingia nchini kwa njia zisizo halali.

Bidhaa hizo ni tani 4.5 za majani ya chai yanayodaiwa  kutumika kutengeneza pombe feki ambayo ni kali.

Nyingine ni mafuta ya kula lita 9,482, mfuko mbadala iliyo chini ya viwango tani saba, sukari tani 4.5, maziwa ya Bruckside lita 186 na vyombo vya usafiri vilivyotumika kusafirisha bidhaa hizo ambavyo ni magari manane, pikipiki 11 na baiskeli moja.

Akizungumza leo Alhamisi Februari 13, 2020  meneja msaidizi wa forodha, Edwin Iwato amesema bidhaa hizo zimekamatwa kuanzia Julai 2019 hadi sasa.

Amesema katika bidhaa hizo, yapo majani ya chai ambayo hutumika kama malighafi ya kutengeneza pombe kali inayotengenezwa kinyemela.

"Yanatumika kutengeneza pombe haramu ambapo huyatumia kutia rangi kwenye spiriti na kutengeneza hizo pombe kali za viwandani jambo ambalo ni hatari kwa afya," amesema Iwato.

Advertisement

Meneja wa TRA Mkoa wa Kilimanjaro, Gabriel Mwangosi amesema bidhaa zote zilizokamatwa zina thamani ya zaidi ya Sh239.9 milioni na zote zinatoka nchi ya  Kenya kwa kupitia njia za panya.

 

Advertisement