TRA yaongeza matumizi stempu za kielektroni bidhaa za aina nne

Kamishna Mkuu wa TRA, Dk Edwin Mhede

Muktasari:

Kwa mujibu wa Tangazo la TRA lililotolewa katika gazeti la Mwananchi jana linaeleza kuwa hatua hiyo inafuatia kukamilika na kuanza kwa matumizi ya mfumo huo kwa awamu ya kwanza na pili.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetangaza kuanza kutumia stempu za kodi za kielektroniki (ETS) katika bidhaa za juisi za matunda na mbogamboga, maji ya kunywa yaliyofungashwa kwenye chupa na bidhaa za filamu na muziki yaani kanda zilizorekodiwa.

ETS zitaanza kutumika katika bidhaa hizo kuanzia Novemba Mosi, 2020 huku ikiwataka wazalishaji wote wenye leseni, waingizaji waliosajiliwa, wasambazaji, wauzaji wa bidhaa zinazotozwa kodi ya ushuru wa bidhaa kuzingatia hilo.

Kwa mujibu wa Tangazo la TRA lililotolewa katika Gazeti la Mwananchi leo Alhamisi Oktoba 22, 2020 na kusainiwa na Kamishna Mkuu wa TRA, Dk Edwin Mhede, linasema hatua hiyo inafuatia kukamilika na kuanza kwa matumizi ya mfumo huu kwa awamu ya kwanza na pili.

Awamu hizo zilihusisha bidhaa za sigara, mvinyo, pombe kali, bia, na aina zote za vileo mnamo  Januari, 2019 na kwa bidhaa za vinywaji laini ilikuwa Agosti 14, 2019.

 “Kutokana na ufafanuzi wa hapo juu, na kwa muktadha wa kutekeleza matakwa ya Kifungu cha 5(1)(a) cha Sheria ya TRA, SURA 399 R.E 2019, wadau wote pamoja na umma kwa ujumla wanataarifiwa kuwa juisi.”

 “Maji ya kunywa yaliyofungashwa kwenye chupa, kazi za filamu kwa mfano, CDs/VCDs/DVDs/ Kanda zilizorekodiwa, zitakazozalishwa ama ndani ya nchi au kuingizwa kutoka nje ya Jamhuri ya Muungano lazima ziwe zimebandikwa Stempu za Kodi za Kielektroniki kama ilivyoelekezwa katika Kanuni ya 4 ya Kanuni,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Pia, imeelezwa kuwa kwa sababu bidhaa hizo hazikuwa zikibandikwa stempu hizi awali, sasa imeelekezwa bidhaa zilizopo sokoni na kwenye maghala ya watengenezaji au waingizaji wa bidhaa hizo ambazo hazijabandikwa ETS zinaruhusiwa kuendelea kuuzwa kwa kipindi kisichozidi miezi mitatu.

“Yaania kabla au hadi kufikia Januari 31, 2021, kama ilivyofafanuliwa kwenye Kanuni ya 44(3) ya Kanuni tajwa, Baada ya tarehe hiyo, bidhaa hizi zote hazitaruhusiwa kuwepo sokoni bila kubandikwa Stempu za Kodi za Kielekroniki,”  inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Kutokana na hilo, kila mzalishaji  na mwingizaji wa bidhaa tajwa anapaswa kutoa taarifa TRA juu ya idadi ya bidhaa alizonazo na hazijabandikwa stempu ETS kabla ya tarehe rasmi ya kuanza matumizi ya mfumo huu kwa kujaza fomu maalum inayopatikana kwenye ofisi za TRA za kila Mkoa na katika tovuti ya Mamlaka.

 “TRA inawakumbushwa wafanyabiashara na wadau wote kuwasilisha taarifa kamili ya chapa zao na idadi ya stempu za ETS wanazokusudia kutumia kwa mwaka ujao ili waweze kusajiliwa katika Mfumo wa Usimamizi wa Stempu za Kodi za Kielektroniki (ETSMS) na kuweza kuagiza stempu kupitia tovuti salama iliyofungamanishwa ndani ya tovuti ya Mamlaka,” imesema taarifa hiyo iliyotolewa na Dk Mhede.