TRA yashauriwa kuendelea kuwekeza kwenye teknolojia za kisasa kukuza mapato

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Dkt. Edwin Mhede akimpa zawadi ya jarida linaloonesha vivutio mbalimbali vilivyopo hapa nchini Katibu Mkuu wa Shirika la Forodha Duniani (WCO), Dkt. Kunio Mikuriya wakati alipotembelea TRA jana jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

Tayari mamlaka hiyo ya mapato Tanzania ili kwenda na wakati na kudhibiti upotevu wa mapato, imeanzisha utozaji wa kodi kupitia stempu za kielektroniki (ETS) zinazodhibiti bidhaa feki sokoni.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imeshauriwa kuendelea kuwekeza kwenye teknolojia ya kisasa kwa kuwa Tanzania ni nchi mojawapo za ukanda wa Afrika Mashariki yenye lango kuu la kuingilia linalosaidia kukuza uchumi kupitia ushuru wa forodha unaotozwa katika eneo hilo.

Ushauri huo umetolewa leo Alhamisi Februari 6, 202 na Katibu Mkuu wa Shirika la Forodha Duniani (WCO), Dk Kunio Mikuriya alipotembelea TRA akiwa kwenye ziara ya kikazi ya siku tatu hapa nchini.

“Ili kusimamia ushuru wa forodha ipasavyo, suala la teknolojia halikwepeki, hivyo ni muhimu TRA ijikite zaidi katika kuendelea kuwekeza kwenye mifumo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwa na watumishi wenye uwezo wa kuendesha mifumo hiyo,” amesema Dk Mikuriya.

Dk Mikuriya ambaye amefanya mazungumzo na mwenyeji wake, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dk Edwin Mhede, wamezungumzia pia umuhimu wa matumizi ya teknolojia katika kudhibiti na kusimamia ushuru wa forodha kwenye bandari ya Dar es Salaam na maeneo mbalimbali hapa nchini.

Hata hivyo, itakumbukwa kuwa tayari mamlaka hiyo ya mapato Tanzania ili kwenda na wakati na kudhibiti upotevu wa mapato, imeanzisha utozaji wa kodi kupitia stempu za kielektroniki (ETS) zinazodhibiti bidhaa feki sokoni.

Mfumo huo wa kidigitali ulianza kutumika rasmi Januari, mwaka jana katika bidhaa za mvinyo, pombe kali na sigara.

Agosti Mosi mwaka huu, TRA ilitangaza kuanza kutumika kwa awamu ya pili ya stempu za hizo za ETS kwa kampuni zinazozalisha vinywaji vya kaboni na vinywaji baridi.

Uamuzi wa matumizi ya stempu hizo yamehitimisha matumizi ya stempu za kawaida katika vita ya kupinga ukwepaji wa kodi na bidhaa feki.

“Suala la bidhaa feki si tu kwamba ni changamoto kwa biashara, bali pia kwa Serikali kwa sababu tunapoteza mamilioni ya kodi na matokeo yake tunashindwa kutekeleza miradi ya maendeleo,” aliwahi kunukuliwa na vyombo vya habari Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi TRA, Richard Kayombo katika mkutano wa kifungua kinywa (staftahi) ulioandaliwa na Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI) katika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam, Septemba 2, 2019.

Takwimu zilizopo nchini hivi sasa zinaonyesha tangu ETS zilipoanza kutumika kwenye tumbaku na vinywaji vyenye kilevi, makusanyo ya ushuru wa forodha yanazidi kuongezeka.

Hata hivyo, Kamishna Mkuu wa TRA katika mazungumzo yao leo na Dk Mikuriya amesema ziara ya Katibu Mkuu huyo imelenga kuimarisha mahusiano baina ya nchi wanachama wa WCO ambaye alikuwa nchini Kenya kwa ajili ya kazi hiyo pia.

“Tanzania ni mwanachama wa WCO na kuna ushirikiano ambayo tunafanya kwa pamoja kuhakikisha eneo la forodha linatekeleza majukumu yake ili kuhakikisha kuna usalama wa bidhaa kwenye eneo la biashara,”  amesema Dk Mhede.

Amesema Tanzania ni kitovu cha biashara kwa kuwa inahudumia nchi zote ambazo hazina bandari kwa mfano Zambia, Malawi, Zimbabwe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambao wote wanatumia Bandari ya Dar es Salaam.

Hivyo, ni muhimu kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa katika kusimamia masuala yote ya kiforodha.

Katibu Mkuu huyo baada ya mazungumzo hayo ameelekea Jijini Dodoma kwa lengo la kukutana na baadhi ya watunga sera kwa ajili ya kuimarisha uhusiano yauliopo.