TRA yasisitiza matumizi ya bidhaa zenye stampu ya kielektroniki

Muktasari:

Mkurugenzi wa TRA wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi, Richard Kayombo amesema TRA imefanikiwa kwa hatua kubwa baada ya kuachana na stampu za karatasi na kuanza kutumia zile za kieletroniki.


Dar es Salaam. Wakati mwaka 2019 ukikaribia ukingoni, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imewataka wananchi kuhakikisha wanananua bidhaa zilizokuwa na stampu za kieletroniki (ETS), kuepuka usumbufu.

Mkurugenzi wa TRA wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi, Richard Kayombo akizungumza na Mwananchi leo Desemba 18, 2019, amesema TRA imefanikiwa kwa hatua kubwa baada ya kuachana na stampu za karatasi na kuanza kutumia zile za kieletroniki.

Amesema kutokana na uamuzi huo, Serikali imepunguza uvujaji wa mapato na kupata kwa wakati kiasi cha kodi kinachostahili kulipwa kama ushuru wa bidhaa, VAT na ushuru wa mapato.

"Ninawasihi wazalishaji wote na waagizaji wa bidhaa nchini kuhakikisha wanatumia mfumo mpya wa stampu za kielektroniki uliowekwa na Serikali kuepusha kukamatwa, pia ninatoa wito kwa wananchi kuhakikisha inapata wito kwetu pindi wanapohitaji ufafanuzi," amesema Kayombo.

Amesema matumizi ya ETS kwenye bidhaa ilianzishwa baada ya kupiga marufuku utumiaji wa stampu za karatasi ambazo zilihusishwa na matukio ya ukwepaji wa kodi na kwa hivyo, kulenga kuboresha ulipaji kodi na kumaliza ukwepaji kodi nchini.

Awali, Serikali ilitangaza mpango wake wa kupitisha mfumo wa stampu za kieletroniki Juni 2018 ambao ulipingwa na wazalishaji nchini kwa madai kuwa utaongeza gharama kwenye uzalishaji.

Kampuni ya Uswizi, Société Industrielle et Commerciale de Produits. Alimentaires (SICPA), ilishinda zabuni na baadaye kusaini mkataba na TRA, kwa ajili ya usambazaji, usanifu na utoaji wa programu itakayoungwa na mfumo wa ETS.

Kufuatia uamuzi huo, wazalishaji walifanya mkutano wa pamoja na serikali kuweka bayana kuwa walikuwa hawapingi mfumo huo ila wanapinga gharama zitakazotokana na ufungaji wa ETS.

Wazalishaji wa bia, vinywaji visivyo na kileo na sigara walidai kuwa zabuni haikutolewa kwa ushindani na kuwa walitakiwa kulipa gharama za ufungaji wa mashine hiyo.

Walisema mfumo mpya unaotumia mihuri ya kidigitali utaongeza ushuru wa bidhaakwa kuwa malipo yatahesabiwa kwa kila kitengo (unit) badala ya kwa lita kama yanavyofanika hivi sasa na hivyo kuongeza mzigo kwa mzalishaji na mlaji wa mwisho.

Kyombo amesema ilionekana kuwa uamuzi huo utaongeza kodi hadi Dola za Marekani 10.1 kwa vitengo 1,000 na kusababisha gharama ya ziada ya Dola za Marekani 100 milioni kila mwaka kwenye viwanda.

Licha ya malalamiko, Serikali ilizindua awamu ya kwanza ya ETS Januari 15, 2019,  mihuri iliwekwa kwenye kampuni 19 ambazo zinazozalisha mvinyo na pombe kali.

Awamu ya pili iliyozinduliwa Agosti 1, ilihusisha vinywaji visivyo na kilevi ikiwamo maji na vinywaji vya kaboneti.

Hata hivyo, baada ya mfumo huo kuzinduliwa, Oktoba 11, kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ilipotembelewa na maafisa wa TRA ilibainisha kuwa mfumo huo unamanufaa makubwa kwa wazalishaji kwa kuwa wanaweza kutambua kwa urahisi bidhaa bandia zinapoingia sokoni.

Mfumo wa ETS unaiwezesha Serikali kutumia teknolojia ya kisasa kupata data ya uzalishaji kwa wakati kutoka kwa wazalishaji.

Wakati huo huo TRA iliendelea kusisitiza kuwa mfumo huo unaiwezesha Serikali kufutilia kwa karibu bidhaa zinapotoka viwandani, vituo vya kuingilia mipakani, kwenye ghala hadi hatua ya mwisho.

ETS imechukua nafasi ya stampu za karatasi kwenye sigara, vileo na vinywaji visivyo kuwa na vileo, dawa, kadi za kucheza, maji ya chupa, vipodozi, leseni na bidhaa zingine. Ina sifa maalum za usalama kama kitambulisho.

Takwimu zilizothibitishwa na TRA zinaonesha kuwa ushuru wa bidhaa na makusanyo ya VAT kwenye bidhaa hizo uliongezeka kwanzia mwaka wa fedha wa 2019/20 ikilinganishwa na kipindi hicho hicho mwaka jana.