TRA yawalima barua wamiliki migodi ya Tanzanite

Muktasari:

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)   imewaandikia barua wachimbaji madini ya Tanzanite Mirerani mkoani Manyara nchini Tanzania wakiwataka kutekeleza sheria na kanuni za ajira na uchimbaji madini.

Babati. Wamiliki 163 wa migodi walioajiri wachimbaji 4,500 wa madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara nchini Tanzania, wameandikiwa barua na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya kuwalipia kodi ya ajira na tozo ya ufundi wachimbaji hao.

Meneja wa TRA mkoani Manyara, John Mwigura akizungumza na waandishi wa habari jana Alhamisi Agosti 15,2019 alisema kati ya wamiliki hao 163 ni 31 pekee waliopeleka taarifa za wafanyakazi walionao na namna wanavyofanya shughuli zao migodini.

"Migodi ya dhahabu kule Geita wanalipa kodi ya ajira kwa wachimbaji wao na tozo ya ufundi hivyo wachimbaji wa madini ya Tanzanite nao wanapaswa kulipa kama wamiliki wa maeneo mengine wanavyofanya," alisema Mwigula.

Alisema kila wakizungumza na wamiliki hao juu ya kuwalipia kodi ya ajira na tozo ya ufundi kwa wafanyakazi wao wamekuwa wakitoa sababu tatu kwa TRA ambazo wanadai hawastahili kuzilipa.

Alisema sababu ya kwanza wanadai hawajaajiri kwenye migodi, pili wameajiri ila hawalipi mishahara na ya tatu hawajapata madini hivyo hawawezi kulipa chochote.

Alisema waliwaeleza kuwa wanapaswa kuwapa taarifa za mrejesho wa wanavyofanya kazi na uzalishaji kila mwezi lakini hawafanyi hivyo wanapeleka kwenye ofisi za tume ya madini.

"Kati ya wamiliki hao 163 wa migodi ni wamiliki 31 pekee walioleta taarifa zao za uchimbaji kwa kila mwezi ila baada ya kuona wamiliki wenzao hawaleti nao wakaacha kutuletea ndipo tukaamua kuwapa taarifa wote," alisema Mwigura.

Alisema endapo wamiliki hao wasipolipia wenyewe kwa hiari watawafikisha mahakamani baada ya kukutana nao Mirerani na kuzungumza nao juu ya malipo hayo kuanzia miaka mitatu iliyopita hadi sasa.

"Timu ya TRA mkoani Manyara itakuwa Mirerani kwa muda wa siku tano kuanzia Agosti 19 hadi 23,2019 kwa ajili ya kuzungumza na wamiliki hao wa migodi juu ya kodi ya ajira na tozo ya ufundi," alisema Mwigura.

Alisema wanafanya hayo kupitia sheria ya madini, sheria ya kazi inayowataka wawe na mikataba ya kazi na sheria ya kodi ya mfumo wa kujikadiria kulingana na wafanyakazi ulionao.

Kwa upande wao baadhi ya wachimbaji hao wamedai kuwa utaratibu wa kulipa mishahara wachimbaji madini haupo hivyo suala la kodi ya ajira na tozo haliwahusu.

Mchimbaji madini Isack John (mwanaApolo) alisema wao wana utaratibu wa kulipwa asilimia 10 pindi madini yakitoka na siyo mishahara kila mwezi.