Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi zatakiwa kuimarisha ukusanyaji kielektroniki

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi nchini Tanzania, Profesa Elisante Ole Gabriel

Muktasari:

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi nchini Tanzania, Profesa Elisante Ole Gabriel amezitaka taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kuimarisha ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielektroniki ili kuweza kutoa gawio serikalini

Dar es Salaam. Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi nchini Tanzania, Profesa Elisante Ole Gabriel amezitaka taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kuimarisha ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielektroniki ili kuweza kutoa gawio serikalini.

Gabriel ameyasema hayo jana Agosti 19, 2019 jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha  kusaidia uboreshaji wa mifumo ya ukusanyaji wa mapato ya serikali kwa njia hiyo.

Gabriel amesema udhibiti wa ukusanyaji wa mapato sehemu zenye minada unaweza kuinua sekta hiyo kimapato tangu walipoanza kuweka udhibiti kuanzia mwaka 2018.

”Mnada wa Maswa ulikuwa ukikusanya Sh756,000 kwa siku lakini baada ya kuweka udhibiti kwa kupeleka wasimamizi mapato yaliongezeka na kufikia Sh7 milioni kwa siku,” amesema Gabriel.

Amebainisha kuwa mnada wa pili wa halmashauri ya Bariadi, mkoani Simiyu baada ya udhibiti mapato yaliongezeka kutoka Sh2 milioni hadi Sh3 milioni kwa siku na kufikia Sh14.9 milioni kwa siku.

Wizara hiyo ilikuwa inatumia Sh44 milioni kwa mwezi kutengeneza na kusambaza vitabu vya risiti katika vituo zaidi ya 400 nchini.

“Nawataka wataalam baada ya kuwa na mifumo imara ya ukusanyaji wa mapato, pia kufikiria na kuona njia nyingine za kuongeza wigo wa ukusanyaji mapato,” amesema Gabriel.

Mkurugenzi Mkazi wa ya Trade Mark East Africa nchini, John Ulanga amewataka watumishi wa wizara hiyo kubadilika kifikra katika utendaji vinginevyo mifumo hiyo ya ukusanyaji mapato haitakuwa na faida yoyote.