Tahadhari ya corona Dar si majumbani tu, hata maeneo ya starehe

Saturday March 28 2020

 

By Ephrahim Bahemu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Unaweza kusema corona imetibua kila sehemu hadi katika maeneo maarufu ya starehe jijini Dar es Salaam nchini Tanzania.

Hiyo ni kutokana na  baadhi ya baa ya kumbi maarufu kufungwa, nyingine kuwa na wateja wachache kutokana na tahadhari ya ugonjwa huo ambao nchini Tanzania watu 13 wameripotiwa kuugua huku ikitajwa kuwa wanaendelea vyema na mmoja kupona.

Jana Ijumaa Machi 28,2020 Mwananchi lilizunguka katika baadhi ya viwanja maarufu jijini Dar es Salaam na kukuta hamna watu waliojitokeza licha ya kuwa ni mwishoni mwa wiki tofauti na kawaida ilivyokuwa kabla ya mlipuko wa virusi vya corona maeneo ambayo ni maarufu kwa starehe kwa wazawa na wageni yamepoa.

Eneo la Masaki hususani ukingoni mwa barabara ya Haile Selasi kuna maeneo mengi ya starehe ambayo ulikuwa ukipita wikendi mida ya jioni unaweza kula bata kwa macho lakini sasa ukipita kumetulia ni kama unapita Barabara ya Ocean/Barack Obama usiku.

Eneo la Life Park (ITV) ambalo ni maarufu kwa baa kwa sasa limepoa ukiingia klabu watu ni wachache na baa yake ya nje hakuna watu, wenyeji wanasema Corona imekimbiza watu.

Kupitia ukurasa wa Instagramu Beach Kidimbwi ambayo ni baa maarufu ilitangaza kusitisha huduma kuanzia Jumatatu ikiwa ni hatua ya kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona hata hivyo wateja maarufu wa kiwanja hicho walisema watu walianza kupungua kwa kasi hata kabla ya tangazo hilo.

Advertisement

“Kutokana na mlipuko wa ugonjwa virusi vya corona unaoenea kwa kasi duniani uatawala wa beachi kidibwa umesitisha huduma kuanzia Machi 23, 2020, tunafanya hivi kwa kutambua kwamba usala wa wateja na wafanyakazi wetu ndiyo kipaumbele chetu,” ilisema taarifa hiyo.

Buckets ambao wapo Masaki pembezoni mwa Barabara ya Haile selas nao walitangaza kufunga biasahara wiki moja iliyopita kwa sababu hiyohiyo kwa lengo la kuepusha kuendelea kwa maambukizi huku wakiwataka wadau wao kuwaombea wagonjwa.

“Katika kipindi hiki cha janga la dunia mawazo na sala zetu zipo kwa wote walioathirika, tunashukuru kwa shangwe tulilokula pamoja na tunaomba na kusali tuvuke salama. Japo kinyonge, sema fresh,” ilisema taarifa ya Buckets kwa wateja wao.

Vilevile kiwanja kiitwacho Havoc nao wametangaza kusitisha biashara kwa sababu ya corona wakisema hatua hiyo imechukuliwa kwa kuzingatia kuwa wamiliki wanajali afya za wateja na wafanyakazi wao.

Katika taarifa yao Havoc waliomba Baraka za Mungu huku wakisema kuwa wana Imani punde wataendelea kula bata na wadau wao. Waliamalizia taarifa yao kwa kuelekeza tahadhari za kuchukua ili kujikinga na virusi hivyo ambavyo mpaka sasa vimewapata watu 13 nchini.

 

Advertisement