Taharuki yatanda baada ya Waziri mkuu Boris kulazwa kwa corona

Muktasari:

Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johson amelazwa hospilani na kuwekewa mashine ya kupumua kwa saa kadhaa baada ya kuzidiwa na ugonjwa wa Covid-19.

London, Uingereza. Taharuki imezuka kwa saa kadhaa jijini London baada ya hali ya Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson kubadilika ghafla na kulazimika kuwekewa mashine ya kumsaidia kupumua.

Waziri Mkuu Boris aliyekuwa katika karantini kwa siku 10 kutokana na kuambukizwa virusi vya corona Jumapili iliyopita alihamishiwa hospitalini baada ya kuendelea kuonyesha dalili za ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa taarifa ya ofisi yake ya Downing Street, Boris alipelewa hospitalini juzi usiku baaada ya ushauri kutoka kwa daktari wake.

“Licha ya kuendelea na matibabu kwa siku 10 bado alionyesha dalili za virusi hivyo pamoja na kuwa na kiwango cha juu cha joto mwilini,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa zilizopatikana baadaye mchana jana kupitia Shirika la Habari la AFP zilisema kuwa afya ya waziri mkuu huyo ilibadilika kwa saa kadhaa na kuwekewa mashine ya kumsaidia kupumua.

Hata hivyo, msemaji kutoka ofisi yake, Robert Jenrick alikaririwa akisema kuwa kiongozi huyo anaendelea vizuri na matibabu.

Jenrick alisema “Waziri Mkuu Boris ataendelea na majukumu yake ya usimamizi wa serikali licha ya kulazwa hospitalini.”

Alisema katika kipindi ambacho Boris amelazwa, Waziri wa Mambo ya Nje, Dominic Raab ataongoza mkutano wa majadiliano ya virusi vya corona.

Hali hiyo inajiri muda mchache baada ya Malkia Elizabeth II kulihutubia taifa akisema kwamba Uingereza itafanikiwa katika vita dhidi maambukizi ya virusi vya corona.

Katika hotuba yake isiyo ya kawaida, Malkia Elizabeth II aliwashukuru wafanyakazi wa afya kwa kujitoa kuhudumia waathirika wa ugonjwa huo.

Malkia Elizabeth alisema mpaka idadi ya walioambukizwa virusi vya corona imepanda na kufikia watu 47,806 na 4,934 walipoteza maisha.

Akizungumza katika jumba la kifalme la Windsor, malkia Elizabeth alisema taifa hilo limekubwa na changamoto nyingi lakini janga la corona ni tofauti.

Katika hatua nyingine, Rais wa Marekani, Donald Trump amemtumia salamu za pole Boris na kumuombea apone haraka.

Rais Trump alituma salamu hizo muda mfupi kabla ya kuanza kwa mkutano wake na waandishi wa habari uliohusu masuala ya corona.

Rais Trump alisema “Wamarekani wote wanamuombea apone haraka na kurudi katika majukumu yake.”