Takukuru Arusha yawapandisha kizimbani 22

Monday January 13 2020

Mkuu wa Takukuru mkoa wa Arusha, Frida Wikesi

Mkuu wa Takukuru mkoa wa Arusha, Frida Wikesi akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Arusha leo. Picha na Filbert Rweyemamu 

By Filbert Rweyemamu,Mwananchi [email protected]

Arusha. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru) mkoa wa Arusha imewafikisha mahakamani watuhumiwa 22 kwa tuhuma mbalimbali za vitendo vya rushwa katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2019.

Mkuu wa Takukuru mkoa wa Arusha, Frida Wikesi akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Jumatatu, Januari 13, 2020 amesema kufikishwa mahakamani kwa watuhumiwa hao kumetokana na ushirikiano  mzuri wa raia wema ambao wapo tayari kutoa ushahidi mahakamani.

Amesema miongoni mwa watuhumiwa hao ni askari polisi, wafanyabiashara na watumishi wa umma na kwamba mashauri yao bado yanaendelea mahakamani katika hatua mbalimbali.

“Katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba mwaka jana zilipokelewa  taarifa 127 kutoka sekta mbalimbali zikiwemo halmashauri 20, elimu(9), mahakama(6), polisi 16, Nida (8), Maji(9), Vyama vya Ushirika 10, Uchaguzi 10 na taarifa binafsi 10,” amesema Wikesi

Ameongeza kuwa katika kipindi hicho Takukuru imefungua mashtaka mapya 11 mahakamani ambapo hadi sasa jumla ya mashauri 45 yanaendelea.

Advertisement