Takukuru yamng’ang’ania hakimu kwa tuhuma ya kupokea rushwa

Muktasari:

Alikamatwa baada ya kudaiwa kuwa alishawishi apatiwe Sh300,000 kutoka kwa mzazi aitwae Juma Mbungi baada ya kumwambia kuwa ametumwa na hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Kishapu, aweze kumsaidia kupata ushindi katika kesi ya kubakwa mtoto wake wa kike iliyokuwa ikisikilizwa katika mahakama hiyo.


Shinyanga. Hakimu mkazi mahakama ya mwanzo  wilaya ya Kishapu Benjamin Charles Mhangwa amekamatwa na taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru) akidaiwa kutenda kosa la kuomba na kupokea rushwa ya Sh200,000 kinyume na kifungu cha 15 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Inadaiwa, awali alishawishi apatiwe Sh300,000 kutoka kwa mzazi aitwae Juma Mbungi kwa kumwambia kuwa ametumwa na hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Kishapu ili aweze kumsaidia kupata ushindi katika kesi ya kubakwa mtoto wake wa kike iliyokuwa ikisikilizwa katika mahakama hiyo.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari mkoani Shinyanga leo Jumatano Oktoba 9, 2019, kaimu Kamanda wa Takukuru mkoa wa Shinyanga, Hussein Mussa amedai kuwa hakimu huyo amekamatwa akipokea fedha taslimu Sh200,000 kutoka kwa Juma Mbugi Septemba 27,2019 ndani ya maeneo ya kata ya Kishapu kupitia kwa Vicent Makolo ikiwa ni sehemu ya Sh300,000 alizoomba.

Mussa amesema uchunguzi uliofanyika umebaini kuwa fedha hizo hazikuombwa na hakimu mkazi mfawidhi wa wilaya ya Kishapu Wilberforce Luwago, hivyo mtuhumiwa huyo ambaye ni hakimu wa mahakama ya mwanzo Kishapu, aliomba na kujipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu.

"Hivyo mtuhumiwa huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani kesho kujibu mashtaka yake," amesema Mussa.

Amewaomba wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kutoa ushirikiano kwa Takukuru katika kuwafichua wale wote wanaojihusisha na vitendo vya rushwa, ili kuweza kuwachukulia hatua za kisheria.

Mwisho.