Tamko la kustaafu Kardinali Pengo waumini wazizima

Muktasari:

Baada ya miaka 27 ya utumishi katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alikuwa akisubiri maombi yake ya kustaafu, ambayo kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis aliyakubali na kutangazwa

Dar es Salaam. Baada ya miaka 27 ya utumishi katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alikuwa akisubiri maombi yake ya kustaafu, ambayo kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis aliyakubali na kutangazwa.

Uamuzi huo ulitangazwa Alhamisi iliyopita wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni, mwili na roho.

Na uamuzi huo, pia umeacha bumbuwazi kwa waumini, ingawa wengi wameona askofu huyo wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam alistahili kupumzika baada ya kazi kubwa ya miaka 27.

Kardinali Pengo, aliyeshika nafasi hiyo mwaka 1992, anamuachia madaraka hayo Askofu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi, ambaye mwaka jana aliteuliwa na Papa kuwa askofu mkuu mwandamizi.

Makardinali ni kama warithi wa kanisa wanaoteuliwa na Papa. Kwa kawaida Papa huteua maaskofu kuwa makardinali ambao huongoza idara za kanisa au episcopal kumsaidia kuongoza dunia. Makardinlai huunda chombo cha kumshauri Papa na huwa na umri chini ya miaka 80 kabla ya kufariki au kujiuzulu.

Lakini wanapokubaliwa kustaafu, huruhusiwa kuendelea na huduma.

“Ataendelea kufanya majukumu mengine ya kumshauri Baba Mtakatifu kwa sababu yeye ni kardinali, kwa hiyo anaendelea tu na huduma,” alisema katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini (TEC), Charles Kitima.

Kwa habari zaidi soma gazeti la Mwananchi la leo Jumapili Agosti 18, 2019