Tamu, Chungu ya mfumo wa stempu za kielektroniki

Muktasari:

Tangu kuanza kwa mfumo huo Mamlaka ya ukusanyaji kodi nchini (TRA) imekuwa ikijivunia mfumo huo na kwamba tayari ukusanyaji wa mapato umeongezeka tangu uanzishwe lakini wazalishaji wa bidhaa wanasema umewaongezea gharama za uzalishaji.

Dar es Salaam. Wazalishaji wa bidhaa wamebainisha kuwa mfumo wa stempu za kielektroniki (ETS) umekuwa na matokeo hasi na chanya tangu kuanza kutumika.

Mfumo wa ETS ambao unatajwa kuwa mwarubani wa udhibiti wa ukwepaji kodi unasimamiwa na kampuni ya Uswis iitwayo Société Industrielle et Commerciale de Produits Alimentaires (SICPA).

Awamu ya kwanza ya mfumo huo ulianza Januari 15, 2019, kwa kuviwekea mfumo huo viwanda 19 nchini vya bia, mvinyo na pombe kali na awamu ya pili ilikuwa kwa vinywaji baridi kama soda na maji na sasa awamu nyingine zinaendelea.

Tangu kuanza kwa mfumo huo Mamlaka ya ukusanyaji kodi nchini (TRA) imekuwa ikijivunia mfumo huo na kwamba tayari ukusanyaji wa mapato umeongezeka tangu uanzishwe lakini wazalishaji wa bidhaa wanasema umewaongezea gharama za uzalishaji.

Kamati ya bunge la bajeti hivi karibuni ilitembelea ofisi ya TRA na baadhi ya viwanda (Sigara (TCC) na kiwanda cha bia cha Serengeti ili kuona namna mfumo huo unavyofanya kazi, ilibaini chunga na tamu ya mfumo huo.

Kamati hiyo ambayo awali ilipingana na waziri wa fedha alipokuwa akitambulisha mpango huo ilisema mfumo huo una manufaa makubwa katika ukusanyaji wa kodi lakini una changamoto zake kwa wazalishaji.

Katika ziara ya kamati ya bunge TCC Mkurugenzi wa sheria na uhusiano wa ndani wa kiwanda hicho Godson Kizila alisema ETS imeleta usawa wa kufanya biashara miongoni mwa wazalishaji lakini imeongeza gharama za uzalishaji kwa upande wao kwa asilimia 319.

“Mfumo umesaidia kupambana na sigara bandia na kujua uzalishaji ukoje uko wapi na unafanyikaje lakini gharama zimekuwa juu, gharama ya stempu imeongezeka tunatumia dola 20 kwa stempu 1000, tofauti na awali ambapo ilikuwa dola 4.77,” alisema Kizila.

“TCC tunatumia Sh13.8 kwa mwaka kwa ajili ya stempu lakini miaka mitano ijayo huenda gharama hiyo ikafikia Sh69 bilioni, Mfumo mpya umeathiri faida ya kampuni, mtiririko wa fedha na gawio kwa wanahisa”.

Kizila alipendekeza kuwa ni aheri gharama ya stempu hizo ikwa Dola 8.55 za Marekani hususani kwa sigara ambazo asilimia 75 ya mali ghafi zake zinapa hapa nchini lakini pia gharama zake zitozwe kwa Shilingi na sio dola.

Mkurugenzi wa uhusiano wa SBL John Wanyancha lengo la mfumo huo ni kulinda Watanzania dhidi ya bidhaa bandia na ukwepaji wa kodi kwa kutoa makadirio hafifu na wao wanafurahia hilo.

Katika ziara hiyo, Naibu Kamishina wa TRA Msafiri Mbibo alisema kuna majadiliano yanaendelea baina ya TRA na wazalishaji, yapo ya ETS na mengine ya kikodi.

Mwenyekiti wa kamati hiyo bunge Mashimba Ndaki alisema watawasilisha maoni ya wadau kwa Serikali ili ishughulikie changamoto zilizopo na baadhi yake zitapelekwa hadi kwenye bunge la bajeti.